Wananchi wamepongeza uamuzi wa serikali ikiongozwa na Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli wa kufufua viwanda vya korosho vilivyokufa ili vijikite katika ubanguaji kwani wameanza kuona matunda ya uamuzi huo. Wakizungumza wakati Afisa Tarafa Mihambwe, Emmanuel Shilatu alipotembelea kuona utendaji kazi wa kiwanda cha Kitama Farmers Group, wananchi hao wamesema kuanza kufanya kazi kwa kiwanda hicho kumezalisha ajira mbalimbali.
“Naishukuru sana serikali ya Rais Magufuli kwa kufufua kiwanda hiki ambapo tumepata kazi. Sasa tunapata pesa ambazo zinatusaidia kujikimu kimaisha. Mwenyezi Mungu ambariki sana Rais wetu mpendwa Dk. Magufuli”. Amesema mbanguaji mmoja.
Kwa upande wake, Shilatu amesema mchakato wa Tanzania ya viwanda umefanikiwa kuzalisha ajira mbalimbali kwa wananchi na kuongeza kuwa;
“Serikali ya Rais Magufuli ipo kazini. Tanzania ya viwanda ipo kivitendo. Ajira mpya zinazalishwa, ubanguaji sasa unafanyika hapa hapa nchini. Raha iliyoje hii kwa watanzania.” Amesema Afisa huyo.