Msajili Mwandamizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Kitengo cha Miliki Bunifu, Suzana Senso amesema BRELA imeanza kutoa mafunzo ya kurasimisha biashara kupitia mtandao jijini Mwanza. Senso ameeleza kuwa mfumo huo utarahisisha usajili wa kampuni na huduma nyingine kwa wafanyabiashara tofauti na ule wa kutumia nyaraka.
“Kwa sasa shughuli ya usajili inaendelea vizuri mkoa wa Mwanza unafanya vizuri katika kutumia huduma ya ORS tofauti na zamani ambapo mwombaji alikuwa anatakiwa kufika yeye mwenyewe katika ofisi zetu zilizopo Dar es salaam”. Amesema Msajili huyo.
Mafunzo hayo yanawashirikisha baadhi ya maofisa biashara, wanasheria, wafanyabiashara kutoka halmashauri zote nane za Mwanza pamoja na wakaguzi wa ndani wa mahesabu. Aidha, baadhi ya washiriki waliopata nafasi ya kuhudhuria mafunzo hayo wameishukuru BRELA kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuweka ofisi yao mkoani humo.