Spika wa Bunge Job Ndugai ametoa wito kwa serikali kuharakisha mchakato wa kuanzisha bima ya afya moja ili watanzania wote wapate huduma wanapohitaji kama ilivyo kwa nchi jirani za Ghana na Rwanda. Ndugai amesema hayo bungeni baada ya majibu ya serikali kuhusu mchakato wa kuanzisha bima hiyo. Katika maelezo yake, Spika huyo amesema Bunge lilishatuma wabunge kutembelea nchi hizo ili kujifunza namna wanavyotumia mfumo huo na kuomba suala hilo lipewe msukumo na serikali ili watanzania wapate huduma.
“Fanyeni kazi usiku na mchana ili ipatikane bima kwa watanzania wote kwa kuwa lina umuhimu mkubwa”. Amesisitiza Ndugai.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile amesema wizara hiyo tayari imeandaa mapendekezo ya kuanzisha bima ya afya moja na kuwasilishwa katika ngazi mbalimbali serikalini.
“Wizara inaendelea na maandalizi ya utaratibu wa kuhakikisha wananchi wote wanakuwa katika mfumo wa bima ya afya na hivyo kuwa na uhakika wa kupata huduma wakati wowote wanapohitajika bila kuwa na kikwazo cha kifedha”. Ameeleza Dk. Ndugulile.