Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Stephen Katemba amesema Halmashauri hiyo imetoa mkopo wa Sh. 244.61 milioni kwa vikundi vya wanawake na vijana katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuwawezesha kuinua mitaji yao.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria inayotaka Halmashauri zote hapa nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake, vijana pamoja na watu walio na ulemavu. Pamoja na fedha hizo, Katemba pia ameeleza kuwa, wametoa pikipiki 66 kwa vikundi sita wanaofanya kazi za kusafirisha abiria na vilevile wametoa vifaa vya kupikia kwa wanawake wanaouza sabuni. Halmashauri hiyo pia imetoa vifaa vya kutengeneza sabuni.
“Wakati wa kutoa mkopo huu pia tumezingatia kigezo cha vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Mheshimiwa Rais, ndio maana ukiwaangalia vijana wetu wa bodaboda wamevaa shingoni, hilo sio pambo tu bali ni kuonyesha umuhimu wake”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mwalingo Kisemba ametoa wito kwa vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo kuwa mabalozi wazuri na kuhamasisha wengine kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali.
“Tunapokusanya ushuru lazima watu wajue kuna makusanyo haya ndio yanakuja tena kuwasaidia kwenye mikopo kama hii maana ndio tunayogawa asilimia 10 kwa ajili ya kukopesha vikundi kama hivi vya leo”. Amesema Kisemba.