Home VIWANDA Mabilioni kujenga kiwanda cha usindikaji nyama

Mabilioni kujenga kiwanda cha usindikaji nyama

0 comment 119 views

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kusindika nyama cha Tanchoice kilichopo Soga mkoani Pwani. Kiwanda hicho kinachojengwa kwa thamani ya Dola za Marekani 5.5 milioni kinatarajiwa kuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati na kimejipanga kuchinja wastani wa ng’ombe 14,000 kwa siku.

Mpina ameeleza kuwa serikali inafanya harakati zote kuwalinda wazalishaji wa ndani na wawekezaji kwa kuchukua hatua kali na kudhibiti uagizaji wa bidhaa zinazohusiana na mifugo. Amewahakikishia wawekezaji hao ulinzi na usalama wa soko huku akisisitiza kuwa nyama na maziwa yasiyo na viwango hayatoingia katika soko nchini.

Waziri huyo amewataka watendaji kiwandani hapo kuhakikisha ujenzi unakamilika hadi kufikia mwezi Septemba na kusema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ujenzi wa viwanda vingine maeneo ya Longido, Morogoro, Chato na Ruvu unafanyika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Rashid Abdilah ameshukuru serikali kwa kudhibiti uagizaji wa bidhaa za mifugo zilizosindikwa na kuelezea kuwa udhibiti wa uingizaji bidhaa hizo unawahakikishia ushindani wa haki na uhakika wa soko la ndani.

Kufuatia zoezi la “Operesheni Nzagamba” jumapili iliyopita, serikali iliteketeza tani 8 za nyama ya nguruwe yenye sumu iliyoingizwa nchini kinyume na Sheria na kuhatarisha maisha ya watu.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter