Mwakilishi wa Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji nchini (EPZA), Grace Lemunge ametoa wito kwa mkoa wa Lindi kuharakisha mchakato wa kutenga na kuandaa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ili kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Lemunge amefafanua kuwa nchi mbalimbali duniani zilizochukua hatua hiyo zimepiga hatua kubwa kwenye sekta ya viwanda na kutaka mkoa huo kutimiza azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati kwa kuwa na maeneo kwa ajili ya shughuli za viwanda.
“Kama taasisi ya uhamasishaji wa uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji kwa mauzo ya nje tunatoa wito kwa Mkoa wa Lindi kumalizia mchakato wa kutenga na kuandaa maeneo ya uwekezaji wa viwanda, kwa kuwa ardhi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika sekta ya viwanda”. Ameeleza Mwakilishi huyo.
Pamoja na hayo, ameongeza kuwa kutenga maeneo hayo kutarahisisha viwanda kujengwa kwa wingi hivyo kuchochea uzalishaji zaidi wa bidhaa na kuinua uchumi wa taifa.
“Utengaji wa maeneo kwa ajili ya viwanda utarahisisha wawekezaji kupatikana kwa kuwa wapo ambao wana teknolojia mpya ambazo hazipatikani nchini, hivyo kutasaidia watanzania kujifunza na kuzitumia”. Amesema Lemunge.