Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema baada ya kumalizika kwa zoezi la kubaini watumishi hewa,serikali italipa madeni yote ambayo yamehakikiwa na kubainika kuwa ni halali. Amesema pia watumishi katika taasisi zote wahudumie wananchi na kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora Majaliwa ameongeza kuwa Rais Magufuli alisitisha malipo hayo ili kupisha zoezi la kubaini watumishi hewa.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, serikali kwa sasa inadhibiti madeni mapya na kwamba kila mtu ana uhuru wa kujiendeleza kitaaluma lakini ni lazima awasilishe barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri. Maombi hayo yakikamilika ndipo muombaji ayawasilishe chuoni.
Waziri Majaliwa pia amesema serikali imefuta utaratibu wa Mtumishi kuandika barua ya kupandishwa daraja au cheo ili kupata malipo mapya huku akitoa onyo kwa wapokea rushwa na watumishi wasio waadilifu kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao mara moja.