Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Gilbert Fossoun Houngbo amefanya mazungumzo na Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam na kueleza kuwa, mfuko huo umetenga Sh. bilioni 127.3 ambazo zitatumika kufadhili miradi ya kilimo nchini kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwakani.
Houngbo, ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu wa Togo, ametoa pongezi kwa Rais Magufuli na serikali ya awamu ya tano kwa ujumla kwa juhudi wanazofanya ili kukuza uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi iliyofadhiliwa na mfuko huo, kuweka mkazo kuhusu umuhimu wa uwekezaji bila kuwa tegemezi, unaolinda utu, unaozalisha kipato kwa wananchi na kujenga misingi endelevu ya kujitegemea.
Rais huyo wa IFAD pia amesema wanasubiri upande wa Tanzania kuainisha maeneo ya miradi ya kilimo ambapo fedha hizo zilizotengwa zitaelekezwa na kuongeza kuwa ana matumaini miradi hiyo itafanikiwa hasa kwa sababu Tanzania ni nchi yenye amani na dhamira iliyonayo serikali kuhusu maendeleo.
Kwa upande wake, Rais Magufuli ameushukuru mfuko huo kwa uhusiano mzuri na Tanzania na kusisitiza ushirikiano huo ulioanza mwaka 1978 utaendelea kudumishwa. Kuhusu fedha zilizotolewa, JPM amehakikisha kuwa zitaelekezwa katika miradi ya kilimo yenye maslahi mapana ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa matumizi ya dhana bora za kilimo katika uzalishaji, kuzalisha mbegu bora za mazao, kutatua changamoto ya masoko ya mazao na kuboresha ufugaji.
Rais Magufuli ameishukuru IFAD kwa kutotoa masharti kuhusu maeneo fedha hizo zinatakiwa kuwekezwa na kuagiza Wizara ya Kilimo kushughulikia mchakato wa kuanisha maeneo yatakayotumia fedha hizo ili kuinua sekta ya kilimo.