Msajili wa Hazina Dk. Oswald Mashindano amesema serikali imeandaa mchakato wa kuunganisha benki ya Twiga Bancorp pamoja na Benki ya Posta (TPB) baada ya Twiga Bancorp kushindwa kujiendesha na hata kuwekwa chini ya uangalizi wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) tangu mwaka 2016.
Mchakato huo ni utekelezaji wa kauli iliyotolewa na Rais John Magufuli mwanzoni mwa mwezi wa tatu wakati akizindua tawi la benki ya CRDB wilaya ya Chato ambapo alisema kuwa serikali haitatoa fedha kusaidia benki ambayo imeshindwa kujiendesha na badala yake, alizitaka benki hizo ziangalie namna ya kushirikiana na zile ambazo zinajiweza.
Benki ya Twiga iliwekwa chini ya uangalizi wa benki kuu mwaka juzi baada ya kuelemewa na madeni hali iliyopelekea benki hiyo kushindwa kujiendesha na mtaji wake kushuka, hali ambayo ilisababisha amana ya wateja wao kuwa hatarini. Jitihada za BoT kuuza benki hiyo ziligonga mwamba baada ya deni lake kufikia Sh. 21 bilioni.