136
Mkutano Mkuu wa 20 wa Wanahisa wa Benki ya NMB (AGM) umepitisha azimio la kulipa gawio la shilingi Bilioni 48 kwa wanahisa ambapo kila Mwanahisa atapata Shilingi 96 kwa hisa. Mkutano huo ulifanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao Ijumaa iliyopita.
Ongezeko hili la gawio lina akisi mafanikio ya kibiashara ya mwaka 2019 na hali nzuri ya ukwasi na mtaji wa benki ya NMB. Gawio lililopitishwa la shilingi Bilioni 48 au Shilingi 96 kwa hisa ni ongezeko la asilimia 45 (45%) ikilinganishwa na gawio la shilingi Bilioni 33 au shilingi 66 kwa hisa lililolipwa mwaka 2018, sawasawa na sera ya benki ya kulipa theluthi moja (asilimia 33.3) ya faida baada ya kodi kama gawio. Nia ni kuendelea kukuza kiwango cha gawio kwa wanahisa mwaka hadi mwaka.
Kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2019, Benki ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi Bilioni 142 ikiwa ni ongezeko la asilimia 46 (46%) kutoka faida ya Shilingi Bilioni 98 iliyopatikana mwaka 2018.
Kuongezeka kwa faida ya Benki kulitokana na kuongezeka kwa mapato ya uendeshaji, kupungua kwa tengo la mikopo chechefu na juhudi za kupunguza matumizi ya kiuendeshaji yaliyopelekea Benki kumaliza mwaka 2019 bila ongezeko la gharama za uendeshaji.
Kutokana na faida kuongezeka, Bodi na Uongozi wa Benki ya NMB umeridhishwa na matokeo chanya yaliyotokana na mapinduzi ya kiteknolojia na kuimarishwa kwa huduma za kibenki katika kipindi cha mwaka 2019. Mapinduzi hayo ni pamoja na uzinduzi wa huduma za kibenki kwa njia za kidigitali kama NMB Mkononi na kwa njia ya mtandao wa intaneti maarufu kama “NMB Direct” huku yakichagizwa na huduma mbadala za kibenki kupitia NMB Wakala.
Uimara wa NMB kama Taasisi ya Fedha ulipelekea Moody kuipa alama ya B1 ambayo imethibitisha kuaminika kwa Benki ya NMB katika soko la mitaji nchini na kimataifa. Benki ina mtaji wa kutosha kwa asilimia 17 (17%) na ina ukwasi wa kutosha hivyo kuthibitisha usalama wa Benki kibiashara.
Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi – Bi Margaret Ikongo, amebainisha kuwa Bodi inataka kuongeza zaidi pato la wanahisa sambamba na kuongeza uwekezaji kwenye Benki.
“Kwa miaka kadhaa sasa NMB imeendelea kuwa imara kwenye sekta ya fedha hasa kimtaji na dhamira yetu ni kuendelea kuimarika zaidi. Ili kufikia mafanikio haya, tunapaswa kuhakikisha tunafanya maamuzi sahihi katika udhibiti wa mabadiliko yoyote ya kimtaji,” anasema Mwenyekiti.
“NMB imejipambanua katika kuendelea kuchangia maendeleo ya uchumi Tanzania kupitia kupanua wigo wa mikopo ya watu binafsi, mikopo ya biashara, kilimo, huduma za bima na mikopo ya ujenzi.” alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna.
Bi. Zaipuna alisema, matokeo mazuri ya mwaka 2019 yanaonyesha juhudi za uongozi wa Benki kuboresha mkakati wake kibiashara unaoweka kipaumbele maeneo matatu yaani, kuongeza amana, kuongeza mapato na ufanisi wa kiutendaji.
Halikadhalika, NMB imejikita katika kusaidia ukuaji kiuchumi wa wajasiriamali wadogo na wa kati (SME/MSMEs), hususan katika sekta ya kilimo kwa kusaidia kuwajengea uwezo kupitia ushauri wa kitaalam katika uwekezaji na mnyororo wa thamani wa kilimo unaopewa usaidizi mkubwa na Taasisi ya NMB Foundation, ambayo inatoa elimu juu ya huduma za kibenki katika ukuaji wa sekta ya kilimo. Ushauri huu wa kitaalam pia unaandama na mikopo na huduma zingine za kibenki kwa wateja wa sekta hizi muhimu haswa kilimo na biashara.
“Sisi ni Benki Bora Tanzania kwa misingi ya Utawala bora, mapinduzi ya kiteknolojia na mifumo ya huduma za kibenki. Haya kwa ujumla wake yanaongoza utekelezaji wa shughuli za kibenki kwa misingi ya kulinda usalama wa akiba na amana za wateja wetu” aliongeza.