Zipo hatua kadhaa anazotakiwa kuchukua mtu yeyote mwenye kuhitaji kufanya biashara au ujasiriamali. Sio tu hatua bali pia anahitaji kuwa na maandalizi kwa maana ya vitendea kazi ili kujihakikishia ufanisi katika kazi. Lipo suala kubwa ambalo limekuwa kikwazo kwa watu wengi hasa vijana wanaojaribu kujiajiri hasa katika nyakati hizi ambazo ajira ni tatizo kubwa.
Mtaji ni kitu chochote ambacho unaweza kutumia katika kuzalisha kitu kingine kwa lengo la kupata faida.
Hivyo basi ili biashara yoyote ianzishwe ni lazima uwe na mtaji.
AINA ZA MITAJI.
Kuna aina nyingi za mitaji ila hapa kuna zile muhimu nazo ni,
1.Binadamu mwenyewe
2.Mtaji wa fedha
3.Kipaji na taaluma
4.Rasirimali
Makala yetu hasa yatajikita kwenye mtaji wa kifedha maana ndipo somo lilipolenga hasa
Mtaji ndio kitu kikubwa hasa kinachoweza kukufanya ukaweza kuendesha biashara zako kwa ufanisi na kwa weledi. Wapo vijana wengi ambao wameonesha uthubutu wa kujiajiri kwa kujishughulisha na ujasiriamali lakiniwameshindwa kufika mbali kutokana na ukosefu wa miundombinu sambamba na ukosefu wa mitaji.
Mara baada ya kutafuta kila mbinu, kuhakikisha wajasiriamali hawa wanajikwamua, hasa maeneo ya mjini yanayotegemea sana biashara kuliko kilimo,walio wengi wa wafanyabiashara hawa wamejikuta wakikimbilia taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo benki wakiamini ndio mkombozi wao wa mwisho kwa lengo la kupata mikopo ili kuendesha biashara zao.
Ni vyema kuangalia sababu zinazopelekea benki nyingi zisikukopeshe mkopo,na je ufanye nini ili uweze kupata mkopo wako kwa urahisi.
Zipo aina kuu mbili za mikopo, mikopo ya Muda Mfupi na ile ya Mkopo Mrefu. Kwa kawaida, muda mfupi wa mkopo unapaswa kulipwa ndani kipindi cha mwaka mmoja. Hizi zinajumuisha mikopo kwa ajili ya kufadhili shughuli za kila siku za kazi na bidhaa za mikopo kutoka kwawauzaji au watoa huduma. Mikopo ya muda mrefu ni ile inayochukua zaidi ya mwaka mmoja. Mara nyingi kikomo cha mikopo hii si zaidi ya miaka saba.
Sababu zinazopelekea Benki zisikopeshe
- Kukosa dhamana- Watu wengi wamekuwa wakikosa fursa ya kupata mikopo katika benki na taasisi nyinginezo za kifedha kutokana na kukosa wadhamini ambao moja kwa moja wanaweza kuhusika au kuwajibishwa endapo mkopaji atakimbia bila kulipa.
- Uwiano wa deni na kipato- Watoaji mikopo wanazingatia pia kiasi unachohitaji kukopa na mapato unayopata kupitia biashara hiyo endapo vina uwiano. Ni jambo ambalo ni gumu kutokea unaingiza kiasi cha Laki tatu kwa mwezi halafu unaenda kukopa mkopo wa milioni tano ukitegemea kuulipa ndani ya mwezi mmoja. Hii inatokana na uhalisia kuwa watu wengi wamekuwa wakichukua mitaji mikubwa na kuanzisha biashara kubwa zenye kuhitaji usimamizi mkubwa ndani ya muda mfupi ilhali huko nyuma wamezoea kuendesha biashara ndogo ndogo. Biashara kama zilivyo hatua mbalimbali za ukuaji wa mtoto nayo inahitaji hatua kadhaa katika ukuaji wake.
- Idadi, mfumo na kiwango cha wateja wako. Benki nyingi huwa zinaingiwa na wasiwasi wa kukopesha katika biashara zinazotegemea chanzo kimoja tu cha wateja wake. Wakopeshaji wengi wanapenda kuona uwepo wa mtawanyiko wa wateja wa aina mbalimbali ambao unaipa mwanya biashara yako kuwafikia watu wa kila namna kuliko biashara inayotegemea mteja mmoja. Hii ni kwa sababu unaweza kumtegemea mteja mmoja mwisho wa siku akaacha kuja au akafilisika tayari biashara yako imekufa hivyo biashara yako itakufa.
- Kukosa pesa ya mzunguko. Benki nyingi zinazitambua na kuthamini wale watu ambao tayari wana sehemu ya kuanzia. Ni vigumu sana kupata mkopo huku kama hauna hata kiasi kidogo kinachoonyesha wapi umeanzia na wapi unatarajia kufika. Hivyo benki wanachofanya ni kama kukuongezea mtaji ili ili uzidi kwenda mbele zaidi.
Baada ya kuangalia sababu zinazopelekea usipate mkopo ni vema pia kuangalia jinsi unavyoweza kukidhi masharti ya kupata mkopo kwa urahisi zaidi kutoka Benki na taasisi nyingine za kifedha ikiwemo SACCOS.
Kupitishwa kwa maombi ya mkopo kwa muombaji hutegemea vile muombaji unavyoielezea biashara yako, na mahitaji yake ya kifedha kwa mkopeshaji. Kumbuka, wakopeshaji wanataka kutoa mikopo, lakini wanaweza kutoa mkopo pale watakapohakikisha kuwa unaweza kulipa. Njia bora ya kukufanya upate mkopo ni kutuma maombi kwa njia ya maandishi huku yakiwa na uhalisia ndani yake pamoja na ushawishi wa kutosha. Vitu hivi vinatakiwa kuwepo kwenye maombi yako ya mkopo.
- Taarifa za Ujumla – Hapa utaweza kuelezea kuhusu jina la Biashara yako, Umri wake tangu kuanzishwa, mtaji ulionao hadi sasa, lengo kuu la kuomba mkopo na kiasi unachohitaji kukopa.
- Maelezo kuhusu biashara yako, ikiwa ni pamoja na Historia na aina ya biashara (maelezo juu ya aina ya biashara, umri wake, idadi ya wafanyakazi, mali yake),Muundo wa umiliki (maelezo ya sheria ya umiliki ya biashara yako pia ni muhimu.
- Taarifa kuhusu soko – Benki na taasisi nyingine za kifedha wanahitaji kujua wateja wako wanapatikana vipi, na unafanya nini kuhakikisha wateja wako wanakuwa ni wa kudumu. ushindani wako katika soko ukilinganisha na wengine, na hatua utakazochukua kuhakikisha unakuwa bora katika utoaji wa huduma,
- Taarifa za kifedha – Taarifa hizi zinajumuishwa na mapato na matumizi kwa mwaka mzima, na kama ndo unataka kuanza wanahitaji kujua umepanga nini kuhusu mapato na matumizi kwa miaka ijayo, dhamana unayohitaji kuweka ili uweze kuchukua mkopo .
Hakikisha kile ulichokusudia kukifanya baada ya kupokea mkopo unakikamilisha na kukifanya kama ulivyopanga kwa sababu pesa ya mkopo inahitaji nidhamu ya juu sana katika matumizi yake.