Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga amesema benki hiyo itaendelea kudhibiti biashara ya ubadilishaji fedha ili kuhakikisha sekta ya fedha haiyumbi. Gavana huyo amesema hayo wakati wa kikao cha kazi kati ya Rais John Magufuli, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wakuu wa mikoa ambapo ameeleza kuwa, BoT inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuimarisha sekta ya fedha.
Prof. Luoga amefafanua kuwa Benki Kuu inayo akiba ya kutosha ya fedha za kigeni ambazo zinaweza kutumika kwa kipindi cha miezi mitano. Mwezi uliopita, BoT ilifunga takribani maduka 100 ya kubadilisha fedha jijini Arusha kwa kushindwa kukidhi masharti ikiwemo kukosa leseni halali.
“Udhibiti utaendelea kuwa mkali. Hii ni moja ya hatua zitakazoendelea, kanuni ambazo zilikuwepo ziliongeza udanganyifu na maduka yakazidi kuongezeka kiholela. Hatuhitaji maduka 100 ya kubadilisha fedha Dar es salaam, kwani kuna benki za kutosha. Tunahitaji maduka ya fedha kwenye sehemu muhimu kama kwenye mahoteli ya kitalii na mipakani”. Amesema Gavana huo.
Pamoja na hayo, Prof. Luoga amewaonya wafanyabiashara wenye tabia ya kuhifadhi fedha kwenye mabegi wanapoenda kulipia bidhaa nje ya nchi na kusema kufanya hivyo ni ukiukaji wa Sheria.