Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Theobald Sabi amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kukuza mahusiano yaliyopo kati yao. Sabi amesema hayo wakati uongozi wa benki hiyo ulipotembelea NSSF na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Erio. Katika mazungumzo hayo, Sabi ameeleza kuwa NBC inajivunia kufanya kazi na shirika hilo kutokana na uendeshwaji wake kuwa wa kisasa.
Akizungumzia ugeni huo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF William Erio ametoa shukrani zake kwa uongozi mzima wa NBC ambapo ameeleza kuwa mbali na benki hiyo kuifanya taasisi hiyo kuwa mteja wake mkubwa, pia imekuwa ikitoa ushauri wa kitaalamu utakaohitajika ili kuboresha zinazotolewa na taasisi hiyo. Mkurugenzi huyo pia amewahakikishia wageni hao kuwa, mifumo ya fedha ya wanachama inaendelea kuimarika na kuwa salama huku matumizi yake yakiwa ni kwa ajili ya maendeleo ya taifa, Erio pia ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kutoa riba ya asilimia tano kwenye akaunti ya makusanyo kutoka kwa wanachama wa taasisi hiyo.
Mbali na NBC, imeelezwa kuwa benki nyingine ambazo zimetembelea NSSF hivi karibuni ni pamoja na UBA, CRDB na NMB ambazo zote zimekutana na shirika hilo kwa ajili ya kupanga mikakati ya namna wanavyoweza kuimarisha mahusiano yao kibiashara.