Soko la jumla la fedha za kigeni kati ya benki za biashara (IFEM) ni muhimu katika soko la fedha za kigeni. Hili ni soko la jumla ambalo linaziwezesha benki za biashara na taasisi za fedha kuuza na kununua (kubadilishana) dola za Kimarekani na Shilingi kati yao.
Soko hili husaidia kuamua kiwango rasmi cha kubadilisha dola dhidi ya shilingi kwa siku husika. Benki Kuu ya Tanzania pia hushiriki kuuza na kununua fedha za kigeni pale ambapo inalazimu.
Wakati mwingine huingilia soko ili kuhakikisha hakuna mabadiliko makubwa sana ya kiwango cha kubadilisha fedha.
Soko la Fedha za Kigeni kati ya mabenki (IFEM) lina kanuni na taratibu zake, ambazo zinaeleza kinagaubaga namna washiriki wote wanavyotakiwa kufanya biashara hiyo. Aidha, washiriki wote katika soko hilo wanatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu ya Tanzania kuhusu miamala waliyofanya kwa siku.
Washiriki wa IFEM ambao wanavunja kanuni na taratibu za soko hilo hufungiwa kushiriki katika kuuza na kununua kwenye soko hilo kwa kipindi maalum. Kufungiwa huko kunahusu tu ushiriki katika soko la fedha za kigeni kati ya mabenki na sio vinginevyo.
Kwa hiyo, kusimamishwa kwa benki tano za Barclays, Exim Bank, UBA Bank, BancABC na Azania kunahusu ushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki tu, yaani IFEM na sio vinginevyo.
Benki hizo zinaruhusiwa kushiriki katika soko la reja reja la fedha za kigeni, kwa mfano kuuza fedha za kigeni kwa wateja wake au kununua kutoka kwao.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
Benki kuu ya Tanzania (BoT)