Home BENKI Taasisi za fedha mkombozi wa wajasiriamali

Taasisi za fedha mkombozi wa wajasiriamali

0 comment 134 views

Taasisi za fedha maarufu kama ‘microfinance’ zinaendelea kuwasaidia watu wengi hususani wajasiriamali katika biashara zao. Taasisi hizi zipo kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaendeleza watanzania kama wamiliki wa biashara na wajasiriamali ambao hawana uwezo au vigezo vya kupata rasilimali mbalimbali za kifedha katika benki ikiwa ni pamoja na kupata mikopo binafsi au ya biashara, bima, kuweka akiba ya fedha nk.

Ni rahisi kuuliza ikiwa taasisi hizi zimejikita katika utoaji wa mikopo kwa watu wa hali ya chini, je watarudisha vipi fedha zao? Kwa ufupi, taasisi hizi zimejenga njia mbalimbali za kuwahasisha wajasiriamali kutumia huduma zao, pia kumekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wateja wao kwa mfano kuhusu uwekaji wa kumbukumbu za kifedha, usimamizi wa kifedha na ujuzi mbalimbali ili kumsaidia mfanyabiashara au mjasiriamali kuendeleza biashara yake huku akirudisha mkopo kwenye taasisi husika.

Ndio maana ni kawaida kusikia taasisi kama FINCA, Yetu Microfinance na nyingine zinatoa elimu kwa wanawake, wajasiriamali na wakulima wadogo. Hii yote ni kuhakikisha kuwa wajasiriamali wa aina mbalimbali wanapata elimu kabla ya kuamua kujiunga na taasisi hizi na hata baada ya kujiunga kuhakikisha wananufaika na sio kurudi nyuma kimaendeleo.

Taasisi hizi hazipo nyuma kuhusu mambo ya kidigitali, hivyo kuwarahisishia wateja wao taasisi nyingi zinatoa huduma zao kwa kupitia mitandao na simu hivyo si lazima wateja kufika katika ofisi zao kwa mfano kwa ajili ya kujisajili, kulipa mkopo au kujua huduma wanazotoa. Leo hii ikiwa unataka kujisajili kwenye taasisi kama EFC, Fanikiwa Microfinance, Yetu Microfinance, L-Pesa Microfinance na nyingine nyingi unachotakiwa ni kuingia mtandaoni na kuandika jina la taasisi husika baada ya hapo utapata maelekezo muhimu kuhusu taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Urahisi huo unawasaidia watu hata waishio vijijini kupata huduma bila kupoteza muda kufuata huduma maeneo ya mbali na hivyo kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2017, asilimia 84 ya wanawake wamekopa mikopo midogo midogo mwaka 2016 na asilimia 60 ya wanawake hao ni wanawake wa vijijini hivyo taasisi kama Brac, zimeendelea kuwasaidia wanawake na vijana kupata elimu, kujiajiri na kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.

Kila kitu kina mazuri na mabaya yake, hivyo hata matumizi mazuri ya taasisi hizi yataleta mapinduzi ya kiuchumi hapa nchini. Ni muhimu kwa wajasiriamali kuwa na malengo. Ikiwa unataka kuchukua mkopo basi tambua mkopo huo utatumika kwa matumizi gani na ni jinsi gani utarudisha.

Uwepo wa taasisi hizi umeendelea kubadili maisha ya wengi ambao hawapo kwenye sekta rasmi. Kupitia mikopo na huduma mbalimbali, biashara nyingi zimeendelea kufunguliwa na fursa za kujiajiri zimezidi kuongezeka. Tunaweza kusema kuwa taasisi za fedha zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter