Afisa Mwezeshaji Kilimo Fedha kutoka TAHA, Angelina Nyansambo ametoa wito kwa wakulima hapa nchini kuacha uoga na kuchangamkia fursa za mikopo na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi mbalimbali za fedha. Nyansambo ametoa wito huo alipokuwa kiwajengea uwezo wakulima wa mbogamboga katika Halmashauri ya Babati na kueleza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, Tanzania inatumia huduma za fedha kwa 17%, Uganda 28%, Rwanda 21% na Kenya ni 40%.
“Ila kama unakopa kwenda kufanya sherehe ndio mbaya au kama unakopa unataka kuongeza mke wa pili hiyo itakuwa mbaya. Lakini ukikopa wakati unaenda kufanya mambo yako ya kilimo na ukafuata kanuni bora, kwa kupiga hesabu ya faida na hasara utafanikiwa. Kabla ya kukopa unatakiwa kufahamu riba yake sio unakopa tu bila kujua marejesho, angalia kama unatengeneza faida kutoka kwenye mkopo sio unakopa halafu unabaki pale pale, na mkulima unatakiwa uwe na tabia ya kujiwekea akiba, sio ubaki kuwaza kukopa tu”. Amesema Afisa huyo.
Aidha, Nyansambo ametaja baadhi ya madhara ya kukosa elimu ya fedha kuwa ni pamoja na kushindwa kufikia malengo, kushindwa kupanua biashara, kuhama biashara pasipo mpangilio, kutofanya kazi kwa ufanisi na kutofikia huduma mbalimbali za kifedha kwa urahisi.
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wamedai wamekuwa waoga kukopa benki kutokana na kushuhudia wenzao wakifilisiwa mali zao huku wakidai kuwa riba inayotozwa kwenye vikundi ni nafuu zaidi kuliko ile inayotozwa benki. Wametoa wito kwa serikali kushusha riba kwenye taasisi za fedha ili wananchi wanufaike na fursa zilizopo na kuinua uchumi wao.