Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Philis Nyembi amesisitiza wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga kuhakikisha wanamiliki vitambulisho rasmi vya biashara ili kutambulika na serikali. Nyembi ametoa rai hiyo wakati akihutubia wafanyabiashara Kata ya Pamba. Wafanyabiashara hao wamekuwa wakivutana mara kwa mara serikali kufuatia kukosa eneo rasmi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
“Kila machinga na mamalishe ahakikishe anapata kitambulisho cha biashara yake, ili aweze kutambulika na serikali kwa kulipa Sh. 20,000, vinginevyo atakayeshindwa kutekeleza hilo hadi muda wake ukapita hataruhusiwa kufanya biashara hiyo”. Amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha, Nyembi ametahadharisha kuwa wafanyabiashara watakaochelewa kupata kitambulisho hicho watatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wakati huo huo, kuwaonya watendaji wote walio na tabia ya kuwatoza fedha kubwa wafanyabiashara kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo amepiga marufuku wafanyabiashara hao kutumia vitambulisho visivyo vya kwao na kusisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kinyume na kanuni na taratibu za Sheria.