Ukifuatilia kwa makini utagundua kwamba kila biashara ambayo imeshindwa ilifanya makosa ambayo yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara. Kama mjasiriamali/mfanyabiashara ni muhimu kuweka hisia zako binafsi pembeni, kuweka mkakati na kuwa na ukomo wa fedha pamoja na muda. Ulimwengu wa biashara unazidi kuwa mgumu kadri siku zinavyoenda hivyo usipokuwa makini huwezi kupata mafanikio na kufikia malengo hayo.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, 80% ya biashara mpya hufa ndani ya mwaka mmoja wakati takribani nusu ya zile zinazoendelea hupotea ndani ya miaka mitano.
Hakuna mfanyabiashara ambaye anapenda kupata majanga haya kwani punde yanapotokea yanarudisha nyuma maendeleo. Ili kuhakikisha kuwa unatimiza malengo na kukuza biashara yako, ni muhimu kuepuka makosa yafuatayo:
- Kuwa na tamaa
- Ikiwa mfanyabiashara atakosa malengo na atawekeza muda mwingi kutamani mafanikio ya wengine, bila shaka biashara hiyo haiwezi kufika mbali. Biashara huitaji msukumo wa hali ya juu ili uweze kujua mahali unapopatia, na wapi ufanye marekebisho ili kufika mbali zaidi. Kama umeamua kufanya biashara, kuwa na malengo na mipango itakayokuongoza. Usiwe mtu wa kuiga ovyo na kukosa msimamo.
- Matumaini yasiyoendana na uhalisia
- Kila mtu anatamani kuwa katika nafasi nzuri kimaisha. Tofauti inakuja kwenye jitihada na uwezo wako kufikia mahali unapotaka. Unapoanzisha biashara yako, usiwe na matumaini makubwa kuliko uwezo wako. Uwezo wako kifedha, kimazingira na kimauzo ni vipengele ambavyo hutakiwi kuviweka pembeni. Mipango yako iende sambamba na hali yako halisi. Ukifanya hivyo inakuwa rahisi zaidi kupiga hatua na kupata maendeleo.
- Kukataa kuwa umeshindwa
- Wakati mwingine mipango yetu kwenye biashara haiendi vile ambavyo tumepanga. Huenda ikawa ni kutokana na sababu zilizo ndani ya uwezo wako, na huendi ikatokana na sababu ambazo hazipo kwenye uwezo wako. Ni muhimu kukubali pale unapoona biashara fulani imekushinda na matokeo yake sio mazuri kuliko kuendelea kutumia fedha na muda mwingi kujaribu kuifufua upya. Kama mambo hayaendi, kubaliana na hali hiyo, jipange upya, fikiria wazo jingine kisha rudi sokoni.
- Kuzoea mafanikio na kujisahau
- Biashara nyingi hufanya vizuri sana pale zinapokuwa changa. Matatizo huanza kutokea pale ambapo mfanyabiashara anataka kukuza biashara yake bila kufanya kazi kubwa kama ile aliyokuwa akifanya awali. Biashara inapopata mafanikio, watu wanazoea, wanakosa ubunifu na wanasahau jitihada kubwa walizowekeza kuifikisha mahali hapo na hali hiyo hupeleka kuendesha biashara kwa mazoea. Kama wewe ni mmiliki wa biashara, hakikisha unaendesha biashara yako kama ndiyo siku ya kwanza kila siku.
- Kupuuza vipaji
- Kuwa mmiliki wa biashara haimaanishi kuwa unaweza kufanya kila kitu. Kama ipi kwenye uwezo wako, ni muhimu kuweka juhudi kubwa kwenye kuajiri watu walio na vipaji kwani wataiwezesha biashara yako kukua zaidi. Ni kweli kwamba hii itakugharimu lakini ni uwekezaji wenye faida lukuki.
Ukiepuka makosa haya, upo katika nafasi nzuri ya kukuza biashara yako. Wekeza jitihada zako kutambua soko lako, kuwa mbunifu lakini pia weka mazoea ya kusikiliza maoni na ushauri wa wateja wako. Vilevile, tumia mitandao ya kijamii kujitangaza na kupanua wigo wako ili kuwafikia watu wengi zaidi.