Ujasiriamali unaendelea kuwa kimbilio la wengi katika harakati za kupambana na ajira. Wananchi wengi wamekuwa wakitambua fursa na kutumia nafasi hiyo kujiajiri ili kumudu maisha.
Japokuwa kundi kubwa la watu wanajikita katika kujiajiri, ni wachache tu ambao wanafikia mafanikio na kutimiza malengo yao. Unaweza kujiuliza, asilimia kubwa wanakosea wapi? Ni vitu gani ambavyo kila mjasiriamali anatakiwa kuzingatia kabla ya kuanzisha mradi wake?
Hapo chini ni mambo matano (5) ambayo kila mjasiriamali anatakiwa kufahamu:
Huwezi kufanya kila kitu mwenyewe
Hakuna mjasiriamali ambaye anapenda kuomba msaada kutoka kwa watu wengine lakini ni muhimu kutambua kuwa huwezi kufanya kila kitu mwenyewe bila msaada wowote. Unaweza kuwa mchapakazi, mbunifu na mwenye malengo makubwa lakini unapofanya kila kitu bila msaada wowote, inaweza kuwa tatizo kwani unakuwa na mzigo mkubwa ambao unaweza kushindwa kubeba siku za mbeleni. Kadri biashara yako inavyokuwa, usisite kuomba msaada na kuajiri watu ambao wana uwezo wa kukusaidia.
Wazo tu halitoshi
Ukweli ni kwamba kila mtu ana wazo zuri la biashara lakini wengi wanakwama katika utekelezaji kutokana na vikwazo mbalimbali. Utekelezaji wa wazo la biashara ndio kitu kinachowatofautisha wajasiriamali duniani kote. Kama unataka kufanikiwa katika sekta ya ujasiriamali, unatakiwa kufanya kazi kwa bidii. Mafanikio hajapatikani kwa sababu ya wazo pekee, unahitaji kufanya mambo mengi ili wazo lako lizae matunda. Wazo lako linatakiwa kuwa mwanzo tu, kama unataka lifanikiwe huna budi kulifanyia kazi usiku na mchana bila kisingizio chochote.
Mapato sio kipimo pekee cha mafanikio
Baada ya kuingiza fedha kidogo, ni rahisi kujisahau. Kwa walio wengi, kipimo kikubwa cha mafanikio ni kuingiza kiasi fulani cha fedha/mapato lakini hii haimaanishi kuwa vitu vingine vya msingi havina maana. Jiulize, unabadilisha maisha ya wanaokuzunguka? Unawasaidia wengine kujifunza (wanaweza kuwa wafanyakazi, wateja, wawekezaji) na kuwa bora zaidi? Kuna vipengele vingine muhimu vinavyoashiria mafanikio mbali na utajiri.
Ujasiriamali sio rahisi kama unavyofikiria
Kama unaamini kila kitu unachokiona katika mitandao ya kijamii, basi ni wakati wa kufikiria mbali zaidi. Hatuwezi kukataa kuwa tunaona jinsi wajasiriamali waliofanikiwa wanavyoishi maisha mazuri, wanavyosafiri sehemu mbalimbali duniani na wanavyotumia gharama kubwa kwenye magari, nyumba nk. Lakini tambua kuwa nyuma ya starehe zote hizo kulikuwa na muda mwingi wa kufanya kazi, kushindwa, kufeli na kukata tamaa. Kama sababu pekee ya kutaka kuanzisha biashara ni kuwa tajiri basi upo katika wakati mgumu. Ukweli ni kwamba mafanikio hayapatikani kirahisi kama unavyoona.
Kuwa makini na unaotaka kushirikiana nao
Kufanya biashara na mtu wako wa karibu (familia, rafiki au mume/mke) kunaweza kusababisha athari kubwa. Hii haimaanishi kuwa wote waliofanya hivyo wameshindwa. Kuna ambao wamefanikiwa kufika mbali. Ikifika muda unahitaji mwenzi wa biashara (Business Partner), chukua muda wako na fanya maamuzi sahihi.
Biashara ni kitu kigumu na unaposhirikiana na mtu wa karibu, muda mwingi ni vigumu kufanya maamuzi sahihi bila kuharibu mahusiano hayo. Watu huwa na mawazo tofauti na mara nyingi hii inapelekea kushindwa kuelewana.
Kuanzisha biashara yako mwenyewe ni kitu kizuri sana katika maisha kwani unapata nafasi ya kuleta mabadiliko katika maisha ya watu wengi na jamii kwa ujumla. Kuna faida nyingi za kuwa na biashara lakini pamoja na yote hayo kuna changamoto zake. Mambo yanapokuwa magumu usikate tamaa na badala yake, fanya kazi kwa bidii zaidi, jifunze kutokana na makosa ya nyuma na kikubwa zaidi omba msaada kutoka kwa watu wengine.