Home BIASHARA Bidhaa bora nguzo ya biashara

Bidhaa bora nguzo ya biashara

0 comment 81 views

Ubora wa bidhaa au huduma ni muhimu ili biashara iweze kuendelea na kuleta mafanikio. Ubora huwafanya wateja kuwa waaminifu na kurudi tena kila wakihitaji bidhaa. Pia kwa mtoa bidhaa au huduma bora, hutengeneza mahusiano ya muda mrefu baina yako na wateja kitu ambacho kila mfanyabiashara anatakiwa kuhakikisha kinatokea.

Watu wanaoshughulika na masoko wanatakiwa kuhakikisha kuwa hawapuuzii ubora kutokana na sababu zifuatazo:

Uaminifu

Ikiwa bidhaa au huduma unayotoa ina ubora unaotakiwa ni rahisi kujenga uaminifu kati yako na wateja wako. Hautakuwa na jambo la kuhofia kuhusu bidhaa zako hivyo kuwa na mamlaka hata ya kuongeza bei kwa sababu una uhakika na mrejesho utakaopata kutoka kwa wateja wako. Wateja wengi hufurahishwa na kampuni ambazo zina mahusiano binafsi mara tu wanaponunua na kufurahishwa na bidhaa hizo. Ni jambo zuri kwa kampuni ambayo ina bidhaa bora kujihusisha zaidi na wateja wao ili waweze kujipatia wateja zaidi.

Mwambie rafiki amwambie rafiki

Inaelezwa kuwa 92% ya watu huamini mapendekezo yanayotoka kwa marafiki na familia hivyo ikiwa bidhaa ina ubora wa juu ni rahisi kupata mapendekezo ya ana kwa ana na  kushirikishana zaidi katika mitandao ya kijamii baina ya marafiki. Ili kuwafikia watu wengi zaidi kampuni inaweza kuandaa kampeni na kuwaambia watu wapendekeze kwa watu wao wa karibu. Kupitia wateja walioridhishwa na ubora itakuwa rahisi kwa wateja wengine wapya kuridhishwa na ubora kabla ya kununua kutokana na maelezo watakayopewa na watu wao wa karibu. Pia kitu kingine ambacho kinaweza kufanyika ni kujibu malalamiko na pongezi zinazotolewa mitandaoni. Ubora wa bidhaa huhusiana na huduma inayotolewa kwa wateja.

Kujiepusha na malalamiko na urudishaji wa bidhaa

Ni dhahiri kuwa bidhaa yenye ubora husababisha wateja kurudi tena hivyo kwa kampuni kutumia muda na fedha nyingi kuhakikisha bidhaa inaingia sokoni ikiwa na ubora wa hali ya juu kutaepusha usumbufu wa kurudisha bidhaa hizo na kupata malalamiko yasiyoisha. Ni muhimu kwa kila kampuni kupima ubora wa bidhaa zao kupitia baadhi ya wateja waaminifu kabla ya kuziingiza sokoni ili kujua kama bidhaa ni bora au kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ili kuweza kuwavutia wateja kwa asilimia kubwa.

Muonekano

Watu hupima kiwango cha ubora kutokana na muonekano wake, inavyosikika, inavyohisi na hata inavyonukia. Hivyo ni muhimu kwa mfanyabiashara kuhakikisha bidhaa ina muonekano mzuri ili kuweza kuwavutia wateja wengi zaidi. Kwa mfano, wauzaji katika mitandao ya kijamii hupata wateja wengi kutokana na muonekano wa picha wanazoweka katika akaunti zao.

Fursa ya masoko makubwa

Kuwa na bidhaa zenye ubora siku zote hukuza soko la bidhaa na kuhamasisha watu kutoka sehemu mbalimbali kununua na ndiyo maana hata kukiwa na fursa za kupeleka bidhaa nje ya nchi, siku zote kiwango cha ubora hupewa kipaumbele zaidi ili kuweza kupeleka bidhaa katika masoko makubwa nje ya nchi.

Uaminifu na ukweli wa mteja aliyefurahia bidhaa huunda mauzo ya kujirudia na kusambaa kwa maoni mazuri, jambo ambalo lina mchango mkubwa kwani husaidia kuwafikia wateja wengine wapya.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter