Shirika la Ndege la Precision Air limetangaza rasmi safari zake mpya za Dar es salaam-Dodoma na Kilimanjaro-Dodoma kuanzia Aprili mosi mwaka huu. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo ya habari imeeleza kuwa, shirika hilo litakuwa likifanya safari sita kwa wiki kuelekea Dodoma ambapo siku za Jumatano na Ijumaa, safari hizo zitapitia Kilimanjaro huku siku zinazosalia safari zikiwa za moja kwa moja.
“Safari zetu hizi mpya zitaiunganisha Dodoma na mikoa mingine kama Mtwara, Dar es salaam, Mwanza, Arusha na Nairobi kupitia Dar es salaam na Kilimanjaro. Abiria kutoka maeneo haya wataweza kuunganisha safari zao kuelekea Dodoma kupitia mtandao wetu wa safari, na hivyo kuunganisha jamii, jambo ambalo ni moja kati ya malengo yetu makuu”. Ameeleza Meneja Masoko na Uhusiano wa Shirika hilo, Hillary Mremi katika taarifa hiyo.
Precision Air ilianzishwa mnamo mwaka 1993 kama shirika binafsi la ndege za kukodi, likiwa linafanya safari za kusafirisha watalii katika vivutio mbalimbali kama vile hifadhi ya taifa ya Serengeti, visiwa vya Zanzibar pamoja na bonde la Ngorongoro. Kutoka Dar es salaam, shirika hilo kwa sasa linafanya safari zake kuelekea Bukoba, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro, Mtwara, Tabora, Kahama, Zanzibar, Entebbe pamoja na Nairobi.