Home BIASHARA Uwekezaji mifuko ya UTT AMIS waongezeka

Uwekezaji mifuko ya UTT AMIS waongezeka

0 comment 107 views

UKUBWA wa Mifuko ya Uwekezaji katika kampuni ya UTT AMIS umeongezeka kutoka Sh bilioni 290.7 Juni 30, mwaka jana hadi kufikia Sh bilioni 412.8, Juni, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS, Casmir Kyuki aliwaeleza wanachama wa mifuko wakati akiwasilisha taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka jijini Dar es Salaam.

Kyuki alisema ongezeko hilo la Sh bilioni 122.1 ni sawa na asilimia 42 ukilinganisha na pungufu ya Sh bilioni 4.4 sawa na asilimia hasi 1.5 kwa mwaka uliopita.

Alisema “Kiwango hiki cha ukuaji wa mfuko ndani ya mwaka mmoja kimefikiwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mifuko ya uwekezaji wa pamoja na kampuni ya uwekezaji ya UTT AMIS pamoja na taasisi zilizotangulia.

Ukuaji wa mifuko pia unadhihirishwa na ongezeko la idadi ya wawekezaji 13,671 sawa na asilimia 9.4 ukilinganisha na ongezeko la wawekezaji 5,169 sawa na asilimia 3.7 mwaka uliopita”.

Alifafanua kuwa mwaka huu wa fedha pato la wawekezaji wa mifuko ni zuri ambapo kwa upande wa Mfuko wa Umoja pato la wawekezaji ni asilimia 10.3.

Kyuki alisema pamoja na changamoto nyingi zilizojitokeza ndani ya mwaka wa fedha uliopita bado mfuko huo umeendelea kufanya vizuri ikilinganisha na mifuko mingine ya uwekezaji.

“Pamoja na changamoto za ugonjwa wa Corona na mabadiliko ya sera za uwekezaji katika nchi zinazoshirikiana na Tanzania, utendaji wa soko bado umeendelea kuwa wa kuvutia na kuridhisha.

Mazingira imara ya udhibiti na jinsi serikali ilivyozifanyia kazi changamoto hizi ndiyo msingi wa kuwa na madhara madogo kwenye utendaji wa soko,” alieleza Kyuki.

Alisema miamala ya uwekezaji kwa njia ya mitandao imekuwa ikiongezeka na kufikia wastani wa Sh milioni 300 kwa mwezi, baada ya huduma hiyo kuzinduliwa Novemba mwaka jana.

“Hili ni ongezeko zuri. Hata hivyo kampuni itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma kwa njia ya mitandao ya simu kwa kuwa tunaamini kuwa bado kuna fursa ya kuongeza miamala zaidi ya hapo tulipofikia,” alisema Kyuki.

Alieleza matarajio ya mwaka wa fedha 2020/2021 kuwa ni kufungua vituo vya huduma kwa wawekezaji katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya pamoja na Zanzibar ambapo mpaka mwisho wa mwaka watakuwa katika mikoa sita ukijumlisha Dar es Salaam na Dodoma.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter