Home FEDHAMIKOPO Bado una madeni?

Bado una madeni?

0 comment 99 views

Kuchukua mkopo si jambo baya ili mradi mkopo huo uwe unakwenda kuzalisha fedha zaidi ambazo zitakusaidia wakati wa mrejesho. Kuwa na mikopo isiyoisha hutokana na kutokuwa na mpango madhubuti wa kulipa mikopo hiyo.

Ikiwa umechoshwa na mikopo isiyoisha jambo la kwanza la kufanya ikiwa unataka kuondokana na mikopo hiyo ni kujua ni kwanini unadaiwa mikopo hiyo, baada ya kujua hilo hatua inayofuata ni kupunguza mikopo hiyo. Ikiwa hujui shida iliyokupelekea kukopa mikopo hiyo basi itakuwa shida kufanya mabadiliko.

Hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea uendelee kuwa na madeni:

Kufikiri una muda mwingi wa kulipa deni lako. Mara nyingi watu hupeana ushauri kuwa si lazima walipe madeni yao kwa uharaka ikiwa wana weza kutumia fedha hizo katika mambo mengine ya kimaisha ikiwa ni pamoja na burudani. Huu si ushauri mzuri. Unaweza kuona una muda mwingi wa kulipa madeni yako lakini jambo muhimu la kujua ni kuwa hujui mambo yanayoweza kutokea kesho. Kwa kusubiria kulipa madeni yako na kutumia fedha katika mambo yasiyokuwa na umuhimu kutakupelekea uwe katika wakati mgumu ikiwa jambo litatokea. Unatakiwa kujiuliza maswali kama; Je nini kitatokea ikiwa utapoteza kazi yako na una madeni? Au nini kitatokea ukiwa una gharama kubwa za matibabu huku umeelemewa na madeni?

Kuchukulia kadi ya mkopo kama sehemu yako ya kipato. Ikiwa unatumia kadi basi hakikisha kuwa unatumia matumizi ambayo mwisho wa mwezi unaweza kuyalipia. Kuchukulia kadi yako ya mkopo ni sehemu yako ya kipato kutasababisha ulimbikize madeni ambayo huwezi kulipa hivyo kujitengenezea historia mbaya ya ukopaji na kusababisha benki kuifungia kadi hiyo. Hivyo ili kuepukana na madeni yasiyo na msingi jitahidi kulipa madeni unayodaiwa katika kadi yako ya mkopo kila mwezi.

Unafananisha hali yako na watu wengine. Watu wengi hupenda kufananisha hali yao ya mikopo na hali ya watu wengine kwa matumaini kwamba watajisikia kawaida na si vibaya. Si vyema kufanya hivyo kwasababu kwanza unatakiwa kujua kuwa mikopo ya watu wengine haikuhusu, kwasababu hujui wamejipangia mipango gani kuilipa mikopo hiyo, au mikopo hiyo inawaumiza kwa kiasi gani.

Unaamini kuwa unastahili vitu unavyonunua. Kila mtu anastahili vitu vizuri lakini ni muhimu kuangalia uwezo wako unapoishia. Kama mtu mwingine amenunua televisheni ya 3D inchi 100, gari la gharama haimaanishi na wewe ununue ili hali huna uwezo huo. Kwa kufanya hivyo unajiingia katika mikopo ambayo huna uwezo wa kuilipa na isiyokuwa na umuhimu.

Kuna njia nyingi za kupunguza matumizi na kuweza kuweka akiba zaidi ambayo itakusaidia kulipa mikopo na kutimiza malengo yako ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi bili zisizokuwa na umuhimu kwa mfano badala ya kununua vocha kila siku nunua kila baada ya mwezi, baada ya kulipia king’amuzi kila mwezi lipia baada ya miezi mitatu au unaweza usilipe kabisa ikiwa hutumii televisheni mara kwa mara. Pia unaweza kutumia bima katika mambo mbalimbali kama afya, gari na biashara ili kupunguza gharama za moja kwa moja.

Ili kutengeneza fedha zaidi na kuweza kulipa madeni unaweza kuuza vitu ambavyo huna matumizi navyo kama nguo, vifaa, vitabu nk. Kama una gari unaweza kujisajili na Uber au Bolt ili uweze kupata fedha zaidi mbali na kazi yako ya mchana.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter