Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya huduma ndogo za fedha nchini.
Sekta hizo ni pamoja na huduma za mikopo ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa na manufaa kwa wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa semina kwa wabunge iliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, amesema kuwa BoT imefanya juhudi kubwa kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI ambapo maafisa maendeleo ya jamii na maafisa biashara wanajengewa uwezo ili kuwatambua wale wanaokopeshana bila leseni na kuwachukulia hatua stahiki.
“Tumetengeneza mwongozo ambao tutatoa mwezi Julai mwaka huu, ukiainisha mambo ya kufanya na adhabu kwa wanaokiuka sheria. katika kila ngazi ya kata na wilaya, wanaokopesha watakuwa na vikao vya kukutana na kupeana taarifa kuhusu wale wanaokiuka taratibu,” amesema Tutuba.
Gavana ameeleza kuwa mikopo mingi inatozwa gharama kubwa zisizoeleweka kama vile ada ya fomu, ada ya kushughulikia mkopo, na ada ya mkopo.
Amebainisha kuwa mwongozo mpya utakaotolewa utadhibiti gharama hizi zote ziwe sehemu ya ada ya mkopo pekee.
“Kuna baadhi ya wakopeshaji wanaweka riba na gharama za bima zisizoeleweka, lakini miongozo itadhibiti gharama za ziada zisiwe sehemu ya mkopo.
Pia, watatakiwa kuwasilisha viwango vyao vya riba BoT kwa ajili ya kuviidhinisha na vitatumika kwa mwaka mzima,” ameeleza Tutuba.
Kwa upande wa wakopaji, Gavana amesema kuwa changamoto kuu ni kutokurejesha mikopo kwa wakati, huku wakopeshaji wakikosa uwazi wanapokopesha.
“Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma, ikiwemo kuingiza mada za elimu ya fedha katika mitaala rasmi ili kuhakikisha watu wanapohitimu shule wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha,”amesema.
Gavana Tutuba amesisitiza kuwa BoT inaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wanaokiuka sheria, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya leseni na kuwapeleka mahakamani.