Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini wa mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, alisema miradi iliyokusudiwa kutekelezwa kupitia fedha hizo ni Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA), uliopatiwa Euro milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 257.64) na utasambazwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara.
Mradi mwingine utakaonufaika na mkopo huo ni Mradi wa Umeme wa Kuunganisha Tanzania na Zambia unaojulikana kama “Tanzania – Zambia Interconnector Project” ambao utagharimu Euro milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 257.64) kwa ajili ya kuchangia uunganishaji wa Mashirika ya Umeme ya Kusini mwa Afrika kwa pamoja yanayojulikana kama “Southern African Power Pool” na Mashirika ya Umeme ya Afrika Mashariki kwa pamoja yanayojulikana kama “Eastern African Power Pool” na Kazi za Nyongeza kwenye Mradi wa Maji Safi na Maji Taka katika miji inayozunguka Ziwa Victoria ambazo zitagharimu Euro milioni 30 (sawa na shilingi bilioni 77.29) na itahusisha maeneo ya Buhongwa, Kisesa na Buswelu katika jijini la Mwanza.
Pia Bw. James alimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kudumisha mahusiano mazuri kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa, uhusiano ambao umefanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za maji na nishati.
Bw. James aliongeza kuwa miradi yote mitatu ambayo imesainiwa mikataba yake inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025, ambayo inaongoza juhudi za kuleta maendeleo nchini hadi mwaka 2025 na kwa sasa inatekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17 – 2020/21.
‘’Malengo ya Dira yetu ni kuinua, kuratibu na kuelekeza juhudi za Watanzania, fikra na rasilimali za Taifa kwenye sekta muhimu ambazo zitawezesha nchi kufikia maendeleo na kuhimili ushindani mkubwa wa kiuchumi unaotarajiwa’’. Alisema Bw.James.
Alilishukuru Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kuwa licha ya kuisaidia Tanzania kiasi cha Euro milioni 230 wameonyesha nia ya kutoa mikopo mingine yenye masharti nafuu na misaada ambayo inafikia jumla ya Euro milioni 721.7, sawa na shilingi trilioni 1.86 ambazo zitatumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo program ya Maendeleo ya umeme jua, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, Uboreshaji wa Huduma za Kifedha kwa ajili ya Kilimo, Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Dar es Salaam (BRT Awamu ya Tano), Mradi wa Usafi wa Mazingira jijini Dar es Salaam, Mradi wa Nishati wa Kuunganisha Tanzania na Uganda na Mradi wa Nishati wa Kuunganisha Tanzania na Zambia.
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo aliwashukuru wahisani hao na kusema kuwa baada ya kukamilika kwa mchako mrefu wa makubaliano kati ya Tanzania na Ufaransa na kupatikana kwa fedha hizo, Wizara yake itatekeleza mara moja miradi hiyo na kuwahakikishia wananchi kuwa miradi hiyo itakamilika kwa wakati uliopangwa.
Profesa Mkumbo aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuwa mstari wa mbele kwa kuthamini rasimali za Tanzania hivyo kuamua maji ya ziwa Victoria kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Awali Mheshimiwa Frederic Clavier, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania alisema mkopo uliosainiwa pamoja na mambo mengine una madhumuni ya kusaidia uendelelezaji wa mradi wa umeme vijijini na utatekelezwa katika Mikoa kumi na sita na kukamilika kwake kutasaidia kuwaunganishia umeme familia zipatazo 90,000.