Home FEDHAMIKOPO Zingatia haya kama unafikiria kuomba mkopo

Zingatia haya kama unafikiria kuomba mkopo

0 comment 115 views

Kila mjasiriamali anahitaji fedha ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kitimiza malengo yake. Kilio cha wafanyabiashara wadogo wengi ni upatikanaji wa mikopo. Mikopo imekuwa kikwazo namba moja kwani taasisi nyingi za fedha zimekuwa ngumu kutoa mikopo hasa kwa wale ambao ndo kwanza wanaingia kwenye sekta ya biashara.

Moja ya vitu ambavyo kama mjasiriamali unaweza kufanya ili kuongeza nafasi ya kupata mikopo ni kuwasilisha ombi la mkopo ambalo linajitosheleza. Unaweza kufuata vipengele vifuatavyo ili kuhakikisha benki au taasisi nyingine za fedha zenye uwezo wa kutoa mikopo zinashawishika kutoa fedha kwa ajili ya biashara yako.

Uandishi wa ombi lenyewe. Kupata au kukosa mkopo huchangiwa na nanmna gani umejieleza katika ombi lako. Jieleze ipasavyo na elezea biashara yako, malengo yako na usiache kuweka taarifa zako muhimu kama vile taarifa za soko, wamiliki,  taarifa za fedha, vibali na leseni. Ni muhimu kwa taasisi kufahamu kuwa unafanya shughuli zako kihalali na Sheria zote husika zinazingatiwa. Jenga uaminifu na ishawishi taasisi kuwa wewe ni chaguo sahihi.

Aina ya Mkopo. Kuna aina mbili kuu za mikopo ambayo ni mikopo ya muda mrefu na ile ya muda mfupi. Kama muombaji ni vizuri kufahamu biashara yako inahitaji mkopo gani kwani masharti hutofautiana. Mikopo ya muda mfupi hulipwa ndani ya mwaka mmoja wakati ya muda mrefu hulipwa kati ya mwaka mmoja hadi miaka saba. Ni muhimu kuangalia aina ya mkopo kulingana na biashara unayofanya na vilevile, uwezo wako wa kurejesha mkopo huo ndani ya muda uliokubaliwa.

Uwezo wako kifedha. Hili ni jambo muhimu kuzingatia wakati unapofikiria kuomba mkopo. Ni vizuri kuweka akilini uwezo wako kifedha ili ikitokea umepata mkopo, unajua jinsi ya kutekeleza mipango yako na kuhakikisha kuwa unarejesha mkopo ndani ya muda uliopangwa bila tatizo lolote. Kufanya hivyo hujenga uaminifu kati ya mkopaji na taasisi. Ni muhimu kutathimini kipato na uwezo wako kifedha ili kuepuka kudumbukia kwenye madeni.

Mpango wa matumizi na marejesho. Wengi wanashindwa kupata au kurejesha mkopo kwa wakati kutokana na kukosa mpango mzuri wa matumizi na urejeshaji. Kabla ya kuwasilisha ombi la mkopo, ni vyema kuandaa mpango ambao utakuelekeza matumizi na mbinu zitakazotumika kwenye marejesho. Unapaswa kuandaa yote haya kabla ya kukopa, usikope kisha uanze kupanga.

Hakikisha unafahamu masuala ya riba. Taasisi za fedha hufanya biashara kwa lengo la kupata faida. Taasisi kama benki hujipatia faida kupitia mikopo. Ni muhimu kuhakikisha kuwa unaelewa kiwango cha riba unachotozwa kulingana na mkopo wako. Wafanyabishara wengi wamejikuta katika hali ngumu kutokana na kutofahamu kuwa mikopo waliokuwa wakichukua ilikuja na riba kubwa. Ili kuepuka hayo, ni vizuri kufahamu riba unayotozwa na kutathmini kama unaweza kuimudu au la.

Mikopo imekuwa msaada mkubwa na imewasaidia watu wengi kutimiza malengo yao na kufika mbali. Pamoja na hayo, imepelekea baadhi ya watu kuwa katika hali Mbaya kiuchumi na wengine hadi kufilisika. Kabla ya kuwasilisha maombi ya mkopo, ni vizuri kufahamu vipengele muhimu vya kuzingatia. Hakikisha fedha unazopata kwenye mkopo zinatumika kukuinua kiuchumi na sio vinginevyo. Unaweza ukapa ushauri kutoka kwa wataalamu wa fedha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuhakikisha mkopo wako unatumika katika mambo ya msingi ambayo baada ya muda, yatakuletea faida.

 

 

 

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter