Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka malengo ya kukusanya shilingi trilioni 30.449 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Kamisha Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda amesema hayo Januari 06, 2025 wakati wa Kikao Kazi cha siku tano kinacho Tathmini Utendaji kazi wa Nusu Mwaka wa TRA kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).
Mwenda amesema kikao kazi hicho, pamoja na mambo mengine kina na malengo kadhaa ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo waliyowekewa na Serikali ya kukusanya shilingi trilioni 30.449 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Akifungua kikao hicho Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza TRA kwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka Tsh. trilioni 22.2 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia Tsh. trilioni 27.6 mwaka wa fedha 2023/2024 na kuvunja rekodi ya kukusanya Tsh. trilioni 16.528 katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 kinachoanzia Julai hadi Desemba Mwaka 2024.
Amesema kuwa fedha hizo zimeisaidia Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za jamii kama vile Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, Mradi wa Treni iendayo kasi (SGR), miundombinu ya barabara, huduma za jamii na mingine mengi.
Dkt. Nchemba ameitaka TRA kuimarisha zaidi mifumo ya kisasa ya kielektroniki ya kukusanya mapato ya Serikali ili kuongeza uwazi, tija na ufanisi kwa kukusanya mapato pamoja na kuziba mianya ya maafisa wa TRA kukutana uso kwa uso na walipakodi.
Aidha, Dkt. Nchemba amerejea wito wake kwa mamlaka hiyo kutofunga biashara za watu wanaowadai kodi badala yake waweke utaratibu wa kuzilea biashara hizo huku wakihakikisha kodi stahiki zinalipwa na wahusika kwa kuwa vitendo vya kufunga biashara vinaathiri uchumi wa nchi pamoja na kuvuruga mfumo wa biashara husika na kuwasababishia watu umasikini na kuwakosesha wananchi ajira.
Dkt. Nchemba alitumia wasaa huo pia kuwataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi, kutumia ipasavyo mashine za kielektroniki (EFDs) na kuwahimiza watoe risiti halali zinazoendana na thamani ya manunuzi yaliyofanyika huku wananchi kwa upande wao wakihimizwa kudai risiti wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.