Licha ya kuwepo kwa janga la Covid-19 ambalo limeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani, mapato ya sekta ya utalii Tanzania yameongezeka kwa asilimia 53.7.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hadi kufikia November 30, 2021 mapato yameongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 1.32 kutoka dola milioni 861.8 mwaka 2020.
Ongezeko hilo, limechangiwa na ufufuaji wa uchumi pamoja na sera rafiki zilizowekwa kwa ajili ya kupunguza athari za janga la Covid-19 ambalo limeathiri uchumi wa dunia nzima.
Kwa mujibu wa BoT, hali hiyo inaonesha kurejea na kuimarika kwa shughuli za utalii pamoja na ongezeko la idadi ya watalii wakimataifa wanaotembelea Tanzania.
Ugonjwa wa Corona, ulisababisha nchi nyingi kufunga mipaka yake huku shughuli za kiutalii zikisimama ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo ambao umeathiri shughuli za kiuchumi duniani.