Wafanyabiashara wametakiwa kujenga tabia ya kuweka akiba katika biashara zao ili kuhakikisha wanakuwa na maendeleo endelevu.
Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ramadhani Myonza ametoa wito huo wakati akitoa elimu ya utunzaji na matumizi sahihi ya fedha katika ziara ya utoaji elimu ya fedha kwa umma wilayani Masasi mkoani Mtwara.
“Kwa mfano mfanyabiashara anayepata shilingi laki moja, anashauriwa kutumia shilingi elfu sitini na kuweka shilingi elfu arobaini kama akiba kwani itamsaidia baadaye, ameeleza Myonza.
Amewaasa wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia pesa zote kwa kisingizio cha kujipongeza, kwani kufanya hivyo kunawarudisha nyuma kimaendeleo.
Akitoa elimu hiyo Myonza amewasisitiza wafanyabiashara kujiepusha na matumizi ya pesa zote wanazozipata na badala yake waweke akiba ya sehemu ya mapato yao.
“Ndugu wafanyabiashara, tujenge tabia ya kujiwekea akiba katika biashara au katika mapato tunayopata katika utafutaji wetu,” amesema Myoka.
Maisha Raimondi, mfanyabiashara kutoka kijiji cha Makanga, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaruhusu wataalam kutoka Wizara ya Fedha kuzunguka mikoani kutoa elimu ya utunzaji na matumizi sahihi ya pesa.
Amesema kuwa elimu hiyo itawasaidia sana wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa mafanikio na kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu.
Katibu wa vikao, Ismail Rashidi, kutoka Kata ya Kilimanihewa, ameipongeza Serikali kwa kutambua kuwa mkoa wa Mtwara kuwa miongoni mwa wanufaika wa elimu hiyo.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi wa Kilimanihewa kuacha tabia ya matumizi mabaya ya fedha na kuwekeza katika taasisi zilizosajiliwa ili kuhakikisha usalama wa fedha zao.