Meneja Mahusiano wa Benki ya NMB kanda ya kaskazini, Christabel Hiza ametoa wito kwa wajasiriamali nchini kuwa mstari wa mbele na kuchangamkia fursa za mikopo ambazo zinatolewa na benki hiyo ili wapate nafasi ya kukuza biashara zao na kuinua kipato. Hiza ametoa ushauri huo wakati akizungumza katika viwanja vya Tangamano mjini Tanga ambapo maonyesho ya wiki ya vijana taifa yanaendelea na kuongeza kuwa, wamekuwa washiriki katika maonyesho yao ili kutoa elimu kwa wateja kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo kufungua akaunti, kununua bidhaa na mikopo inayopatikana ili kuwasaidia kukuza mitaji ya biashara zao.
“Vijana wakiweza kujiunga kwenye vikundi vidogo vidogo wanaweza kupewa elimu ya utawala bora ambayo itawawezesha kukopesheka hatua inakaayowasaidia kuweza kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao za kujiingizia kipato”. Amesema Meneja huyo.
Pamoja na hayo, Hiza ameeleza kuwa wanatoa elimu na kuhamasisha kuhusu mpango mpya wa NMB unaofahamika kama “Kliki” ambao unatoa fursa kwa mteja ambaye anajiunga nao kuweza kupata huduma za kibenki kupitia simu ya mkononi.