Home KILIMO Acheni kurusha mbegu: Mwanri

Acheni kurusha mbegu: Mwanri

0 comment 132 views

Balozi wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Aggrey Mwanri amewataka wakulima wa zao la pamba katika wilaya Bariadi mkoa wa Simiyu kulima zao hilo kwa kutumia vipimo vipya vya kisasa.

Vipimo hivyo ni sentimeta 60 kutoka mstari hadi mstari na sentimeta 30 kutoka shimo hadi shimo.

Mwanri amewataka wakulima kufuata vipimo na kuachana na mtindo wa zamani wa kurusha mbegu.

Ameeleza hayo wakati akitoa semina elekezi ya namna ya kuongeza tija kwa kutumia vipimo vipya katika zao hilo kwa wakulima mbalimbali wa Wilaya.

Amesema kuwa mabadiliko hayo ya vipimo yatamwongezea mkulima idadi ya miche kutoka 22,222 ya awali alipokuwa anatumia vipimo vya sentimeta 90 kwa sentimeta 40 hadi kufikia miche 44,444 kwa kutumia vipimo vipya.

Mwanri amebainisha kuwa endapo wakulima watatumia vipimo vipya wakati wa kupanda zao la Pamba ifikapo mwaka 2025 wanatarajia kuzalisha kiasi kikubwa cha zao hilo na Tanzania inaweza kuwa ya kwanza barani Afrika kwa uzalishaji wa pamba.

Amesema “kama wakulima wakifuata maelekezo na kanuni bora za kilimo cha zao la Pamba kwa kupanda shamba zima kwa kutumia vipimo na kuachana na mtindo wa kupanda mstari wa mbele kwa kufuata vipimo alafu wanaendelea kumwaga mbegu kama zamani hatutafikia malengo tuliyojiwekea.”

Ameeleza kuwa Pamba ni zao muhimu la kimkakati na kibiashara ambalo linachangia takribani asilimia 10 hadi 20 ya pato la Taifa.

Kutoka na umuhimu huo, alisisitiza kuwa wakulima hawana budi kulima zao hilo kwa kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kupambana na wadudu waharibifu kwa kutumia viuatilifu.

Amesema kuwa Bodi ya Pamba tayari imeishachukua hatua mbalimbali ya namna ya kuwasaidia wakulima kupata viuatilifu vitakayowasaidia kupambana na wadudu waharibifu shambani.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter