Home WANAWAKE NA MAENDELEO Rais Samia ataja changamoto maendeleo ya wanawake

Rais Samia ataja changamoto maendeleo ya wanawake

0 comment 41 views

Rais Samia Suluhu Hassan amesema maendeleo ya wanawake yamekuwa yakiathiriwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa rasilimali, kutengwa, kutopata haki na kutopewa nafasi katika kufanya maamuzi.

Rais Samia ameyasema hayo katika Kongamano la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (African Women Leaders Network – AWLN) uliofanyika Zanzibar Desemba 2 hadi 4, 2022.

Amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha wanawake kwa kuhakikisha inatanua mtandao wa wanawake katika sekta mbalimbali.

“Lengo la kuwashirikisha wanawake ni kuweza kufikia Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2021 idadi ya wanawake walioajiriwa ilishuka ambapo wanawake milioni 45 duniani waliondoka katika ajira na hivyo kuwafanya kuwa maskini zaidi.

Amebainisha kuwa Tanzania inafanya jitihada ya kuwashirikisha wanawake katika vyombo vya kufanya maamuzi akitolea mfano kuongezeka kwa idadi ya Wabunge wanawake kutoka asilimia 21.5 mwaka 2005 hadi kufika asilimia 37 mwaka 2022 na Mawaziri 9 katika Baraza la Mawaziri.

Katika kongamano hilo, viongozi wakuu wa nchi za Afrika wamesema bado Afrika inapaswa kuongeza nguvu kuwainua wanawake kiuchumi na kuwaondolea vikwazo.

AWLN ni mtandao ambao unataka kuhakikisha kuwa wanawake wana sauti katika nyanja zote za maisha kwa kutekeleza Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kufikia Malengo ya AU ya kufikia Afrika tunayoitaka.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter