Home KILIMO Bajeti kilimo kufika Trilioni 1 mwakani

Bajeti kilimo kufika Trilioni 1 mwakani

0 comment 181 views

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuifanya nchi kuwa ghala la chakula duniani.
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akishiriki, mdahalo wa viongozi wa ngazi ya juu wa nchi za Afrika, kuhusu chakula na kilimo, ulioandaliwa na Taasisi inayojihusisha na uhamasishaji wa masuala ya kilimo Barani Afrika (AGRA), kando ya mikutano ya Kipupwe iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) jijini Washington D.C, Marekani.

Amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka wastani wa shilingi bilioni 250 hadi kufikia shilingi bilioni 950 katika bajeti inayotekelezwa hivi sasa na kwamba mwaka ujao, bajeti hiyo itaongezwa ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuifanya sekta hiyo kuwa na tija.

“Mwaka ujao wa fedha tutaongeza tena bajeti hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni moja na kuwekeza kwenye miundombinu ya kilimo ambayo tunaamini itaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuishirikisha sehemu kubwa ya jamii wakiwemo vijana ambao kupitia program ya BBT (Build Better Tomorrow), iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu imelenga kuwakusanya vijana na kuwapatia ujuzi wa masuala ya kilimo” amesema Dkt. Nchemba

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iliyoko chini ya Wizara ya Fedha na Mipango Frank Nyabundege amesema kuwa Benki yake imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 500 katika kuendeleza kilimo nchini Tanzania kwa kuwawezesha wakulima wa kati, wakubwa pamoja na taasisi kadhaa zinazojihusisha na kilimo na kwamba juhudi hizo zitaendelezwa kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGRA, ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, ameisifu Tanzania kwa mikakati inayoichukua ya kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuwahusisha vijana na kwamba mpango huo unatakiwa kuigwa na nchi nyingine barani Afrika.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter