Ili mazao yastawi ipasavyo yanahitaji maji ya kutosha. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa mkulima anaweza kulima shamba kwa matumaini kwamba mvua ya kutosha itanyesha na kukuza mazao yake lakini hali ikawa tofauti. Ni muhimu kuwa na njia mbadala na kama tunavyoona hivi sasa, kilimo cha umwagiliaji kimekuwa mkombozi wa wananchi. Mkulima anaweza kumwagilia kwa mikono na chombo cha kuhifadhia maji kama ndoo, au kwa pampu ya mkono au inayotumia umeme au mafuta. Vilevile kuna njia ya kisasa zaidi ya kumwagilia kwa matone.
Umwagiliaji kwa njia ya matone ni nini?
Huu ni mfumo wa kisasa ambao hutumika kumwagilia mazao ambapo kwa kupitia mabomba au mipira yenye matundu madogo madogo maji hupelekwa polepole moja kwa moja katika mmea karibu na mizizi yake.
Faida ya kumwagilia kwa njia ya matone
- Mkulima akitumia njia hii hutumia maji kidogo, kuliko akimwagilia kawaida hivyo kupunguza magugu katika shamba kwasababu matone humwagilia mmea pekeake na si shamba zima.
- Majani yatakuwa yakibaki makavu kwa sababu matone humwagilia mizizi peke yake hivyo kupunguza magonjwa katika mazao.
- Pia kupitia njia hiyo ongezeko la chumvi kwenye ardhi litapungua, na mmomonyoko wa udongo katika shamba utapungua au kuisha kabisa.
- Kama mkulima hutumia pampu kumwagilia, akianza kutumia njia hii atapunguza gharama za kuendesha shughuli nzima ya kumwagilia kwa pampu kwa mfano manunuzi ya umeme, au mafuta na kama hutumia pampu ya mkono akianza kutumia njia ya matone ataweza kufanya shughuli nyingine huku mazao yanaendelea kumwagiliwa na hatochoka.
Hasara za umwagiliaji kwa njia ya matone
- Njia hii ina gharama kuliko njia za kawaida za umwagiliaji, hivyo sio kila mkulima anaweza kumudu njia hii hasa wakulima wadogo.
- Kwa sababu mipira ni ya plastiki, inaweza kuoza na wakati mwingine matundu ya mipira hiyo yanaweza kuziba hivyo mimea kukosa maji na kukauka.
- Wakati madawa yanapuliziwa katika mimea, huhitaji maji katika matawi ili yaweze kufanya kazi na kwa sababu njia hii imelenga kumwagilia mizizi peke yake, dawa hizo zinaweza zisifanye kazi vizuri.
- Mfumo huu unahitaji mtu makini, na mwenye elimu kuhusu umwagiliaji wa aina hii. Tofauti na hivyo, mkulima anaweza kupata hasara kubwa.
- Uharibu wa mfumo kutokana na wadudu.
Mkulima anashauriwa kupata elimu kabla hajaanza kutumia aina hii ya umwagiliaji ili aweze kunufaika zaidi na kuepuka kupata hasara.