Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema muda umefika kwa mataifa ya barani Afrika kuweka bajeti inayojitosheleza kwa ajili ya wataalamu wanaofanya utafiti kwenye kilimo. Waziri huyo amesema hayo jijini Arusha wakati wa mkutano wa kimataifa wa uzindizi wa mradi wa Avisa na kuongeza kuwa, imefika wakati wa nchi za Afrika kuweka bajeti ili kuwawezesha watafiti na kuchochea upatikanaji wa mbegu bora, ambazo zitasaidia kuwainua wananchi kiuchumi.
“Ni wakati mwafaka kwa nchi za Afrika kutenga fedha nyingi na kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija na mapato sambamba na kukusanya kwa wingi fedha za kigeni zitokanazo na mazao ya kilimo”. Amesema Waziri Hasunga.
Pamoja na hayo, Hasunga pia amesema kuwa kilimo ni kimbilio la nchi nyingi Afrika, na kwa upande wa hapa nchini, sekta hiyo inachangia 29.1 katika pato la taifa na watanzania wengi wanakitegemea kwa biashara na vilevile chakula.
Aidha, ametaja baadhi ya changamoto katika sekta hiyo barani Afrika kuwa ni pamoja na matumizi ya jembe la mkono, matumizi ya pembejeo, miundombinu duni, ukame na wadudu.