Wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) amewataka wakulima kuzingatia uzalishaji wa mahindi bora ili kuweza kupata soko hasa la ndani hususani kwa kipindi hiki ambapo msimu wa kununua mazao umeanza. Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA,Vumilia Zikankuba amesema nchi ina chakula cha kutosha hivyo kwa msimu huu wa kwanza wa ununuzi bei ya NFRA itakuwa wastani wa Sh. 380 hadi Sh. 400 kwa kilo.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuzalisha mahindi bora licha ya kupata soko la ndani pia huchagiza kupatikana kwa soko la nje na huepusha chakula kinachohifadhiwa kuharibika kwa muda mfupi.
”Haiwezekani kutumia pesa za serikali kununua mahindi yasiyokizi vigezo na viwango vya serikali hasa yasiyo na ubora na machafu”. Amesema.
Kuhusu elimu kwa wananchi juu ya uzalishaji wa mahindi bora, Zinkakuba alisema elimu hiyo imeshatolewa kupitia vikundi vya wakulima na vyombo vya habari na tayari matunda yameanza kuonekana kwa baadhi ya maeneo kama makambako,sumbawanga na mpanda wamezalisha na kuuza mahindi yenye ubora kwa NFRA. Aliongeza kuwa lengo la serikali ni kwenda uchumi wa kati wa viwanda hivyo mahindi bora ni muhimu kwani hayatumiki kwa chakula pekee bali kutengenezea bidhaa mbalimbali hivyo upatikanaji wa malighafi zenye ubora ni muhimu.
Kuhusu viwango vya mahindi, Zikankuba alisema viwango vya unyevunyevu vinatakiwa kutozidi asilimia 13.5,takataka asilimia 0.5 na punje zilizovunjika zisivuke asilimia 2.
NFRA ni taasisi ya serikali yenye jukumu la kutunza chakula kwa ajili ya dharura hasa majanga kama mafuriko na mengineyo yanayofanana na hayo.