Home KILIMOKILIMO BIASHARA Mzani wa kidigitali wazinduliwa

Mzani wa kidigitali wazinduliwa

0 comment 89 views

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amezindua matumizi ya Mizani za Kidigitali iliyounganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) itakayoimarisha utendaji na uendeshwaji wa Vyama vya Ushirika nchini.

Silinde amesema kuwa vyama vyote vya ushirika wa mazao nchini vitumie mizani ya kidijitali iliyounganishwa na Mfumo wa Upimaji wa Mazao katika kutekeleza majukumu yao.

Silinde ameeleza hayo katika Wilaya ya Tandahimba, Mkoani Mtwara wakati akizindua mizani hizo na kugawa mbegu za mbaazi kwa wakulima wa Wilaya ya Tandahimba.

Amesema baada ya uzinduzi ni kusimamia na kuhakikisha viongozi na watendaji wote wa Vyama vya Ushirika, wanasimamia matumizi sahihi ya vipimo pamoja na matumizi ya mizani ya kidijitali iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo nchini.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Mkoa wa Mtwara una Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) 726 ambavyo vinajishughulisha na mazao ya korosho, ufuta na mbaazi pamoja na vituo vyake vya kukusanyia vipatavyo 2,236.

Vituo hivyo vitahitajika kutumia Mfumo wa Upimaji wa Mazao ya Wakulima uliounganishwa na mizani za kidijitali.

Dkt. Ndiege ameeleza kuwa, wanatarajia kusambaza kompyuta mpakato (Laptop) 726 kwa AMCOS zote zitakazofikishiwa Mizani kwa lengo la kuwezesha na kurahisisha utendaji kazi hususan katika kuwahudumia wakulima.

Amesema matarajio ya Serikali ni kuwa mizani itasaidia kupunguza malalamiko ya wakulima kupunjwa kilo za mazao yao na kuwezesha upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi na kwa wakati.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter