Home KILIMOKILIMO BIASHARA Serikali yadhamiria kumaliza tatizo la mafuta

Serikali yadhamiria kumaliza tatizo la mafuta

0 comment 138 views

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta nchini.

Waziri Mkuu amesema mageuzi hayo yatakwenda sambamba kwa kupanda miche mipya ikiwemo ya michikichi.

Amesema hayo akiwa Mkoani Kigoma na kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wenye ardhi inayokubali zao hilo wafanye hivyo mara moja kwani mbali na kuwapa fedha za uhakika, litaleta fursa ya ajira kupitia viwanda vinavyofunguliwa.

“Mkakati wetu ni kuacha kabisa kuagiza mbegu nje na kuzalisha mbegu wenyewe,” amesisitiza.

“Chikichi ni fursa, chikichi ni maendeleo, ni fursa ya kuleta viwanda hapa Kigoma na kwenye mikoa mingine itakayolima zao hili, chikichi ni uchumi,” ameeleza Waziri Mkuu.

Ameutaja mkoa wa Kigoma kama mkoa wa kimkakati kwa kuwa unazalisha asilimia 80 ya chikichi yote nchini.

Serikali ilichukua hatua za makusudi za kuliingiza zao la michikichi katika orodha ya mazao ya kimkakati, mazao mengine ya kimkakati ni pamba, alizeti, kahawa, korosho, chai, mkonge, zabibu na tumbaku.

Amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kulima mchikichi kutokana na faida zinazopatikana.

Nae Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amesema Wizara hiyo inaendelea na uzalishaji wa mbegu na miche bora ya michikichi aina ya TENERA inayotoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na Wakulima kwa takribani asilimia 90.

Akizungumzia suala la mikopo kwa ajili ya wakulima, Mavunde amesema mpaka sasa tayari Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeidhinisha Sh. bilioni moja na milioni 400 kwa ajili ya wakulima.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter