Na Mwandishi Wetu
Wakulima wa ndizi wilayani Rungwe mkoani Mbeya wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa soko la kimataifa ili kuongeza ushindani na kuwathibiti wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipanga bei kiholela na kuwanyonya wakulima. Hivi sasa wakulima hao wanakosa soko lenye manufaa baada ya wafanyabiashara kupunguza bei kutoka Sh.6000 hadi Sh.4000 kwa mkungu mmoja.
Wakulima hao wameshauri wataalamu kuwapa elimu ya usindikaji ambayo itawasaidia kuepusha hasara wanayopata hivi sasa kwani mazao yao hukaa muda mrefu bila soko. Wameongeza kuwa wamekuwa wakijitahidi kuzalisha zaidi lakini hawanufaiki kwani hakuna wanunuzi wa uhakika huku wachache waliopo wakijipangia bei ambayo inakuwa ndogo kuliko gharama walizotumia kuzalisha.
Serikali pia imetakiwa kuweka mipango stahiki ili wakulima waweze kupata mikopo na pembejeo za kilimo hivyo kufanya kilimo chao kwa ufanisi zaidi na kufikia lengo la uchumi wa viwanda kama serikali inavyotaka. Naye Mkuu wa Wilaya ya Rungwe. Julius Chalya amesema katika harakati za kukabiliana na changamoto hiyo, eka mbili zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo litakalosaidia wakulima kunufaika na kilimo chao.