Kumekuwa na jitihada zinazoendelea kujaribu kukinusuru kilimo kwa kusambaza mbegu bora. Juhudi hizi hasa zimeelekezwa kwenye mazao ya chakula Kama vile mahindi, viazi na mtama. Baadhi ya kampuni zinasambaza mbegu na kuwasimamia wakulima wa mazao yanayotengeneza bidhaa zao mfano bia. Mashirika ya kimataifa nayo yanatoa msukumo wake kuhakikisha Afrika inakuwa na mchango unaostahili katika kujitosheleza kwa chakula.
Juhudi hizo pia zipo kwenye kilimo na usindikaji au ukamuaji wa alizeti nchini. Kwa upande mmoja, jitihada hizi zimekusudia kuvilinda viwanda vya kukamua na kusafisha mafuta ya alizeti visizidiwe nguvu na kumezwa kabisa na vile vya kusafisha na kusindika mafuta ghafi ya mawese ambayo uagizaji wake kutoka nje umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
Uagizaji huu umekuwa ukihatarisha uhai na ustawi wa alizeti pamoja na kilimo cha michikichi nchini. Hata hivyo, jitihada za maboresho hayo kwa kiasi kikubwa yametokana na msukumo na ushawishi wa wafadhili kuliko jitihada zetu wenyewe.
Hili linasababisha mipango mingi kutokuwa endelevu mara tu wafadhili wanapojitoa au misaada ya kufadhili mradi kukoma. Mifano ipo mingi nchini. Kwa kipindi kirefu, kilimo cha alizeti na mbegu nyingine za mafuta ya kula kimegubikwa na maneno yenye nadharia zaidi kuliko sayansi, bila ya mipango thabiti yenye tija na utekelezaji.
Mipango mingi imekosa ufuatiliaji wa karibu na kwa kiasi kikubwa, utekelezaji wake katika maeneo kadhaa ulibakia kwenye karatasi kutokana na changamoto mbalimbali kwa kukosa mifumo shirikishi kukiendeleza kilimo cha alizeti nchini.
Pamoja na umuhimu wake kiuchumi na kibiashara, zao la alizeti kwa kipindi kirefu limekuwa likipuuzwa na kuchukuliwa kama moja ya mazao ya kukumbukwa wakati wa njaa au shida.
Umuhimu wa kibiashara umeelekezwa kwenye mazao yaliyozoeleka mfano pamba, tumbaku, chai, korosho, karafuu, mkonge, pareto na kahawa. Alizeti imeshaulika kiasi cha kutopangiwa mikakati na malengo ya kuliendeleza. Kilimo cha alizeti kwa kiasi kikubwa kinaendeshwa na wakulima wadogo, kimekuwa kikifanywa kwa kubahatisha kutokana na sababu mbalimbali hivyo kuwa na mavuno hafifu na kiwango kidogo cha mafuta katika mbegu zake.
Wakati kwingineko duniani kukiwa na jitihada za makusudi za kuboresha na kuongeza uzalishaji wa alizeti na ukamuaji wa mafuta bora zaidi ambayo ni salama kwa kwa matumizi ya binadamu (kama mafuta ya kupikia), jitihada kama hizo zinakosekana nchini kwa kipindi kirefu sasa.
Hivi karibuni wamejitokeza wafadhili ambao wamejipanga kuwajengea uwezo wakulima kuweka msisitizo kwenye kilimo hiki hivyo kuanza kutoa mwelekeo wa kuliendeleza zao hili katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
Lakini mchango huo wa wafadhili bila ya jitihada za makusudi za Serikali na taasisi zake kusimamia utafiti wa mbegu bora, upatikanaji wa mbegu hizo kwa bei nafuu au kwa mikopo yenye ruzuku na udhibiti wa wanunuzi wakati wa mavuno ya mbegu hizo kabla ya usindikaji hautakuwa na maana yoyote.
Ipo haja kwa wadau kuunga mkono jitihada hizi kwa kurahisisha upatikanaji wa mashine za teknolojia ya kisasa katika kukamua mafuta na kuyasafisha ambazo itakuwa nafuu zaidi zikipata msamaha wa kodi na upatikanaji wa vifungashio vyenye ubora wa kimataifa.
Mamlaka husika zinatakiwa kuongeza umakini na uwajibikaji kama ile ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) au Shirika la Viwango nchini (TBS) kudhibiti uchakachuaji wa mafuta kwa kufuatilia kwa karibu uwezekano wa kuchanganywa na mawese kwa lengo la kutengeneza faida kubwa kwa njia za mkato.
Umakini unahitajika pia katika kudhibiti uwiano wenye tija baina ya uagizaji na uingizaji wa mafuta ghafi ya mawese kutoka nje na kiwango cha uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini kwa kudhibiti kiasi cha alizeti ghafi zinazouzwa nje ya nchi.
Serikali inapaswa kujenga mazingira rafiki kwa wakulima na wadau wengine wa kilimo cha alizeti na wasindikaji wake kwa kuondoa tozo, ushuru na kodi ambazo ni kikwazo kwa sekta hiyo kuongeza ushindani wake katika soko la kimataifa. Vilevile idhibiti mianya ya rushwa katika uingizaji wa mafuta ya mawese na kuhakikisha sehemu kubwa ya yanayoingia inatumika kwa ajili ya kutengenezea bidhaa zitakazouzwa nje na kidogo kinachobaki kitumike kusafisha mafuta ya kupikia nchini kwa kuwa na vifungashio maalum.