Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema Jeshi la Wananchi Tanzania lipo tayari kusafirisha korosho hadi jijini Dar es salaam kwa kutumia meli yenye uwezo wa kubeba tani 500 za korosho baada ya maghala mkoani Mtwara kujaa.
Jenerali Mabeyo amesema hayo katika kikao chake na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mtwara na kueleza kuwa ameshuhudia korosho kujaa kwenye maghala hayo alipofanya ziara na kwamba iwapo korosho zitaendelea kukusanywa, Jeshi litalazimika kutumia meli ili zao hilo liweze kuhifadhiwa Dar es Salaam.
Aidha, Mkuu huyo wa majeshi amesema watalazimika kufanya mazungumzo na wizara ya kilimo ili kujadili namna ya kuandaa maghala hayo na kuhifadhi korosho. Kuhusu ubanguaji, Jenerali Mabeyo amesema vikundi vya wabanguaji wadogo vitatumika na keleza kuwa kinachohitajika ni kuongeza idadi ya watu ili kazi hiyo ifanyika haraka na kwa tija.