Kufuatia sintofahamu ya wakulima wa mkoa wa Kilimanjaro kuhusu zao lenye soko la uhakika, watafiti wamewathibitishia kuwa zao la fiwi lina soko la uhakika na kuwasisitiza kulima zao hilo kwa wingi. Fiwi ni aina ya maharage jamii ya kunde na hulimwa sehemu zenye ukame huku zikistahimili ukavu kwa muda mrefu.
Mtafiti Mwandamizi wa mazao yanayovumilia ukame na mbegu bora nchini, Dk. Mary Mgonja, amethibitisha kuhusu zao hilo wakati akitoa mrejesho kufuatia utafiti walioufanya katika kijiji cha Mabilioni kilichopo wilaya ya Same, ambapo amesema kuwa zao hilo lina manufaa makubwa katika upande wa uchumi na uwezekano wa kustawi zaidi katika wilaya nne mkoani humo.
“Utafiti wa majaribio nilioufanya kuanzia mwaka 1993 hadi sasa, umeleta mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi wa kijiji cha Mabilioni kilichopo wilaya ya Same. Wakulima wa ukanda wa Tambarare wa wilaya ya Same, Mwanga, Moshi na Hai tunawashauri kufanya zao hilo la fiwi kuwa zao kuu la biashara”. Amesema Dk.Mgonja.
Mtafiti huyo ameongeza kuwa ukiachana na zao hilo kuhimili ukame, mkulima anatumia gharama kidogo katika uzalishaji tofauti na ilivyo kwa mazao mengine ya biashara. Pia imeelezwa kuwa soko kuu la zao hilo ni Kenya ambapo fiwi hutumika kutengeneza biskuti na vilevile nchini India ambapo zao hilo hutumika kwa chakula.