Home VIWANDA Hakuna kiwanda kitakachofungwa: Waziri Kijaji

Hakuna kiwanda kitakachofungwa: Waziri Kijaji

0 comment 156 views

Waziri wa Uwekezaji , Viwanda na Biashara , Dk Ashatu Kijaji amesema serikali imedhamiria kuona viwanda vyote nchini vinafanya kazi kwa siku zote saba za wiki.

Ameongeza kuwa hakuna kiwanda kitakachofungwa kwa kushindwa kujiendesha kutokana na masharti ya uwekezaji au kukosa masoko ya bidhaa wanazozalisha.

Dk Kijaji amesema hayo alipotembelea kiwanda cha 21 st Century Textile LTD kilichopo eneo la Kihonda viwandani  Mkoani Morogoro.

“Niseme kwanza hakuna kiwanda kitakachofungwa katika serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, vingine vilivyofungwa  vitaanza kufanya kazi tukianza na kiwanda cha nguo cha kilichopo mkoa wa Mara, ” amesema.

Dk Kijaji amesema serikali inawahitaji wawekezaji kuongeza uzalishaji na kutoa ajira zaidi kwa Watanzania kikiwemo  kiwanda hicho ambacho zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wake ni wanawake .

Amebainisha kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na kiwanda hicho kutatua changamoto mbalimbali zilizowasilishwa zikiwamo za umeme na maji.

Ameeleza kuwa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)  ya mwaka 2020-2025 imeitaka serikali kuendeleza viwanda vilivyopo na kufufua vilivyokufa ili kuweza kutengeneza ajira kwa Watanzania.

amewataka wenye viwanda kuzalisha nguo zenye ubora wa viwango vya  soko la kimataifa na kusisitiza kuwa serikali  imeweka mazingira mazuri  kutumia  soko huru la Marekani  kutokana na juhudi za Rais Samia.

Meneja wa Utumishi na Utawala wa Kiwanda hicho, Nicodemus Mwaipungu amesema hadi sasa  kimetoa ajira za kudumu zaidi ya 2,400 kwa Watanzania.

Ameiomba serikali kusaidia kupambana na waingizaji haramu wa bidhaa za nguo ambao wamekuwa wakiuza kwa bei ndogo na kusababisha kiwanda hicho kutofanya bishara iliyotarajiwa.

“Lengo ni kufikia  ajira 3,000 lakini kutokana na changamoto za maji, umeme pamoja na ushidani wa kibiashara tumeweza kutoa ajira 2,400” ameeleza.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter