Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa watanzania kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere kwa kuwekeza katika viwanda kuwezesha taifa kurudi katika uchumi wa kutegemea uzalishaji unaotokana na bidhaa za viwandani. Samia ametoa ushauri huo katika uzinduzi wa wiki ya maonyesho ya viwanda yanayofanyika mkoani Pwani ambapo ameeleza kuwa mkoa huo una viwanda 429 ambavyo kati ya hivyo, kuna vikubwa, vya kati na vidogo ambavyo vimejengwa huku vingine vikiwa tayari vimeanza uzalishaji japokuwa kuna changamoto za soko la bidhaa hizo kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa kuliko mauzo.
“Tunategemea maonyesho haya yatakuwa endelevu kwa sababu viwanda hivi vinatoa ajira kwa watanzania ni matumaini yangu kuwa wafanyabiashara mtatumia fursa hii kukuza biashara zenu, tulipotembelea baadhi ya viwanda wamiliki wageni wanataka kuondoka na kuachia uongozi na uendeshaji kwa wazawa. Nasisitiza kuendelea kuwepo kwa mshikamano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na sekta binafsi ili uwekezaji ukue zaidi ya hapa na bidhaa zinapouzwa nje na zikiwa na nembo yenye kuonyesha ni bidhaa zilizotengenezwa hapa nchini ni fursa yetu ya kujitangaza”. Amesema Makamu wa Rais
Aidha, Samia ameshauri wizara na sekta zinazosimamia masuala ya kazi na ajira kutembelea viwanda hivyo ili kuona jinsi wafanyakazi wanaendesha kazi zao na kujua kama haki zao kwa mujibu wa sheria zinafuatwa.