Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kulima zao la muhugo kwa wingi kutokana na uwepo wa kiwanda cha kuchakata zao hilo mkoani Lindi.
Majaliwa amesema hayo wakati akifungua kiwanda cha uchakataji mihogo cha Cassava Starch of Tanzania Corporation Limited (CSTC) kilichopo kijiji cha Mbalala mkoani Lindi na kueleza kuwa, pamoja na kutoa ajira, serikali ya awamu ya tano inahamasisha ujenzi wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kupelekwa sokoni.
“Kama unataka pesa nenda kalime muhogo kwani kuna soko la uhakika na pia zao hili ni la muda mfupi na kilimo chake ni rahisi. Kwa sasa hatuna muda wa kukaa vijiweni vijana jiungeni katika makundi na muanzishe mashamba ya mihogo soko lipo tena mwenye kiwanda atawafuata huko huko shambani”. Amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba ametoa pongezi kwa wawekezaji hao kwa kujenga kiwanda cha kuchakata muhogo hapa nchini kwani wamesaidia wakulima kupata soko la uhakika na vijana wengi kuajiriwa.