Serikali imechukua Sh. 3 bilioni ambazo hapo awali zilitolewa kwa Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kimkakati wa machinjio ya kisasa wa Vingunguti, kufuatia Manispaa hiyo kushindwa mradi huo wa zaidi ya Sh. 8.5 bilioni kwa wakati. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, amechukua hatua hiyo baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambapo amesema kuwa, serikali ilitoa Sh. 3 bilioni kati ya Sh. 8.5 bilioni kwa ajili ya kukamilisha mradi Mei 2018, lakini hadi sasa, fedha hizo hazijatumika.
“Fedha haziwezi kukaa kwa mwaka mzima bila matumizi ilihali kuna maeneo mengine ambako fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hivyo tunazichukua fedha hizi na Manispaa ya Ilala mtalazimika kuomba upya mtakapokuwa mmejipanga. Tumewapatia fedha mmeshindwa. Tutazichukua fedha hizi mpaka hapo Manispaa ya Ilala watakapoleta mpango kazi unaotekelezeka na sio huu ambao hawakujiandaa” alisisitiza Dkt Kijaji
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala Ando Mwankuga amekubali kuwepo na ucheleweshaji wa kuanza kutekeleza mradi huo.
“Ucheleweshaji huu si wa makusudi bali ilikuwa ni kuhakikisha tunafuata taratibu zote za ununuzi na kuhakikisha kuwa mradi utakaojengwa uwe na ubora unaotakiwa na unaolingana na thamani ya fedha na tunatarajia kuanza kuutekeleza Machi 10, 2019”. Amesema Mwankuga