Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Suleiman Kakoso, amesema kuwa Kamati yake imefurahishwa na kasi ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), yenye urefu wa Kilomita 300 unaoanza jijini Dar es salaam hadi Morogoro. Kakoso ameeleza kuwa Bunge litaendelea kupitisha bajeti ya mradi huo hadi utakapokamilika.
“Kamati imekagua mradi na imeridhika na hatua za ujenzi wa reli hiyo hakikisheni unakamilika kwa viwango vinavyokubalika na ukabidhiwe mwishoni mwa mwaka huu kama mkataba unavyoelekeza”. Amesema Kakoso.
Mbunge wa Moshi Mjini ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Jafari Michael, amesema mradi huo utaleta mapinduzi makubwa kiuchumi kwa sababu reli hiyo inapita katika mikoa sita inayojitosheleza kwa uzalishaji wa chakula. Vilevile kupitia reli hiyo, nchi itanufaika kwa kupata mizigo kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi na Kongo na hivyo kuchangia katika pato la taifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema ujenzi wa reli hiyo umekamilika kwa asilimia 64 na kuwataka wananchi walio karibu na mradi kutunza reli hiyo ili iweze kutumika kwa miaka mingi zaidi. Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano itaendelea kutekeleza sera zake ili kukuza uchumi wa nchi.