Kampuni ya umeme kiganjani inatarajia kuzindua mfumo ambao utaruhusu wananchi kununua na kupata huduma ya umeme kwa mkopo kutoka Shirika la umeme Tanzania (TANESCO). Kwa mujibu ya Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Fedy Felician, huduma hiyo inayofahamika kama “Kopa umeme kiganjani mwako” ikianza kufanya kazi, itamruhusu mtu kukopa umeme ikiwa hana fedha kwa wakati huo.
Mtendaji huyo pia ameeleza kuwa hadi sasa, kampuni hiyo tayari imepitia taratibu zote ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na serikali, Mamlaka yaudhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura), TANESCO pamoja na kupata hatimiliki kutoka Chama cha Hatimiliki Tanzania (COSOTA).
“Tumefanya uchunguzi mbalimbali kwa jamii tunayoishi na kugundua kuwa kuna mahitaji makubwa ya umeme kwa ajili ya shughuli mbalimbali na hii huduma itasaidia mambo mengi ikiwemo sehemu za biashara”. Amesema Felician.
Mbali na hayo, Mtendaji huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa, kampuni hiyo ya kizalendo imejipanga kusaidia jamii ya kitanzania na kwamba, watashirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampuni za simu na benki ya CRDB na kwamba tayari mazungumzo yameshafanyika.