Serikali ya Tanzania imeazimia kuacha kusafirisha korosho ghafi ifikapo mwaka 2026/27.
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema hayo Agosti 21, 2023 wilayani Mkuranga alipotembelea kiwanda cha TANCOM kinachojihusisha na ukamuaji mafuta ya maganda ya korosho (CNSL) na kiwanda cha SABAYI INVESTMENTS cha kubangua korosho.
Ameeleza kuwa mkakati wa Serikali ni kubangua korosho zote zinazozalishwa nchini ifikapo mwaka 2026/2027.
“Hii sio tu itaongeza kipato kwa wakulima na halmashauri zetu, bali utaongeza fedha za kigeni na ajira kwa wananchi wa Taifa letu.
Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha mkakati huo wa kubangua korosho zote nchini unafikiwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika uongezaji thamani ya mazao ya kilimo na kutatua changamoto za kimsingi za wabanguaji korosho,” amesema Mavunde.
Amebainisha kuwa maelekezo na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona ukuaji wa sekta ya kilimo unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, na ndiyo maana ameongeza bajeti ya kilimo kufikia bilioni 970 mwaka huu wa fedha yaani 2023/2024.
“Moja ya eneo kubwa tulilolipa kipaumbele kama Serikali kupitia Ajenda 10/30 ni uongezaji wa thamani ya mazao ili kuondokana na kuuza yakiwa ghafi.
Kwa upande wa korosho, tayari ekari 1,575.5 katika kijiji cha Maranje Wilayani Nanyamba-Mtwara zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kongani kubwa ya viwanda ambavyo vitakuwa na uwezo wa kubangua tani 300,000 kwa mwaka.
Navipongeza viwanda vya TANCOM na SABAYI INVESTMENTS kwa uwekezaji huu mkubwa wa lengo la kuiongezea thamani korosho yetu.
Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega kuhakikisha lengo kuu la kuuza korosho iliyobanguliwa linafikiwa, amesema.
Akitoa taarifa kuhusu uwekezaji wa kiwanda cha TANCOM, Meneja Uendeshaji Erick Mkanda amesema kiwanda hicho kinachomilikiwa na wawekezaji kutoka nchini Korea kina uwezo wa kuchakata tani 8000 za maganda kwa mwaka na ujenzi wa kiwanda kingine cha kubangua korosho tani 6000 kwa mwaka unaendelea.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Sabayi Investment Ltd, Daniel Marwa amebainisha kuwa mwaka 2019 uwezo wa kiwanda ulikuwa ni kubangua tani 1000 ambapo baada ya kufunga mitambo ya kisasa, kwa sasa wana uwezo wa kubangua tani 10,000 za korosho kwa mwaka, na wameweka lengo la kufikia uwezo wa kubangua tani 40,000 miaka mitatu ijayo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika uongezaji wa thamani wa zao la korosho.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Khadija Nassir ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweka mkazo katika uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza wilayani Mkuranga kwani fursa ni kubwa.