Mtaalamu wa Kilimo kutoka Msumbiji, Jaime Gado amesema Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zinazalisha mchele wenye thamani ikilinganishwa na mataifa ya Kenya, Burundi, Rwanda na Msumbiji. Gado amesema hayo akiwa hapa nchini pamoja wataalamu wa zao la mpunga waliokuja kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana mawazo na wakulima wa Tanzania ili kuzalisha mpunga bora.
“Tumeona changamoto kadhaa, lakini bado mkulima huyu amekuwa akizalisha kilicho bora, tatizo ni uhakika wa soko, naishauri Mamlaka husika kuangalia namna ya kumsaidia mkulima huyu ili pia aweze kuuza kwa wingi katika nchi zinazozunguka bara la Afrika. Nipende pia kuwapongeza Shirika la Maendeleo la Kitaifa la Japan (JICA) kwa kuweka utaratibu wa kuongeza thamani ya zao hili kwa kusaidia kusimamia makubaliano kati ya wanunuzi na wakulima kwa wakulima wa Tanzania kupitia kwenye mradi wa Tanrice 2 kwani umekuwa mkombozi wa wakulima wengi hususani waliopo kwenye skimu ya Lower Moshi”. Ameeleza Mtaalamu huyo.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa hapa nchini Shedrack Msemo ametaja baadhi ya changamoto wanazokutana nazo wakulima kuwa ni pamoja na ukosefu wa mashine bora na ubovu wa miundombinu.